1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yanukovych akubali kujizulu kwa waziri mkuu

28 Januari 2014

Rais Viktor Yanuckovych amekubali ombi la kujiuzulu kwa Waziri Mkuu Mykola Azarov, masaa kadhaa baada ya Waziri Mkuu huyo kutangaza kujiuzulu kwa kile alichokiita kuwezesha mchakato wa kupatikana muafaka wa kisiasa.

https://p.dw.com/p/1AyVZ
Rais Viktor Yanukovych wa Ukraine.
Rais Viktor Yanukovych wa Ukraine.Picha: AFP/Getty Images

“Nimekubali kujiuzulu kwa Mykola Azarov na kwa hivyo kujiuzulu kwa serikali nzima ya Ukraine.” Inasomeka dikrii iliyochapishwa jioni hii kwenye mtandao wa Rais Yanukovych.

Hata hivyo, Rais Yanukovych amelitaka baraza zima la mawaziri kubakia madarakani kama serikali ya muda hadi serikali mpya itakapoundwa.

Mapema asubuhi ya leo, Azarov alitangaza kujiuzulu wadhifa wake, akisema hatua hiyo inadhamiria kufungua njia zaidi za kupatikana kwa muafaka wa kisiasa.

Tayari mshirika huyo muhimu wa Rais Yanukovych alikuwa ameshaahidi mabadiliko ya baraza la mawaziri mwezi uliopita, baada ya bunge kukataa kuunga mkono kura ya kutokuwa na imani na serikali yake.

Azarov ametolewa sadaka?

Wachambuzi wa mambo wanaichukulia hatua ya leo ya kujiuzulu kwa Azarov kwamba ni hitimisho la uvumi uliokuwa umezagaa kwamba Yanukovych alikuwa tayari kumtoa sadaka rafiki yake huyo wa karibu, ili kuwaridhisha waandamanaji wanaompinga.

Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Mykalo Azarov.
Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Mykalo Azarov.Picha: Sergei Supinsky/AFP/Getty Images

Mwishoni mwa wiki, Rais Yanukovych alikuwa hata amependekeza kiongozi wa upinzani na waziri wa mambo ya nje wa zamani, Arseniy Yatsenyuk, achukuwe nafasi ya uwaziri mkuu, na kiongozi mwengine wa upinzani, Vitali Klitschko, awe naibu waziri mkuu, lakini wote wawili wamekataa, huku Klitschko akiapa kutojiunga na serikali yoyote chini ya Rais Yanukovych.

Katika hatua nyengine inayoonekana kulenga kuwatuliza waandamanaji, mchana wa leo (tarehe 28 Januari) bunge lilipiga kura ya kuziondoa sheria tisa mpya, ambazo zimekosolewa kwa kubana upinzani na uhuru wa kujieleza. Wabunge walitazamiwa pia kupitisha sheria ya msamaha kwa waandamanaji.

Hata hivyo, Waziri wa Sheria Yelena Lukash, amesema msamaha huo utatolewa ikiwa tu waandamanaji wataondoka kwenye majengo yote ya serikali na mitaa wanayoishikilia.

Tayari waandamanaji wameondoka kwenye jengo la wizara ya sheria, lakini wametoa wito wa kuyavamia majengo yote ya serikali hadi wenzao wote waliokamatwa waachiliwe huru.

Sheria ambazo zimefutwa leo, zilipitishwa na bunge hilo hilo tarehe 19 Januari na kusainiwa na Rais Yanukovych siku moja baadaye. Kiasi cha waandamanaji wanne waliuawa wiki iliyopita wakati polisi wakitekeleza sheria hizo mpya.

Makamu wa Rais wa Marekani, Joe Biden, alizungumza kwa simu na Rais Yanukovych jioni ya jana, na kumuelezea uungaji mkono wa Marekani kwa mazungumzo yanayoendelea.

Kamishna wa Sera za Ujirani wa Umoja wa Ulaya, Stefan Fule, ambaye kwa sasa yuko mjini Kiev, amesema hivi leo kwamba bunge la Ukraine linapaswa kufungua njia ya mchakato wa kisiasa kumaliza mgogoro huo.

Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/AFP
Mhariri: Josephat Charo