1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Mkuu wa Ukraine ajiuzulu

28 Januari 2014

Waziri Mkuu wa Ukraine amewasilisha barua ya kujiuzulu akisema anapigania muafaka, huku bunge likikutana kuutatua mkwamo wa kisiasa katika nchi hiyo iliyogawika kati ya wanaotaka mafungamano na Ulaya na wanaopinga.

https://p.dw.com/p/1AyH9
Waziri Mkuu wa Ukraine Mykola Azarov.
Waziri Mkuu wa Ukraine Mykola Azarov.Picha: Sergei Supinsky/AFP/Getty Images

"Nimechukua uamuzi huu mwenyewe kumuomba rais wa Ukraine kukubali ombi langu la kujiuzulu kwenye wadhifa wa waziri mkuu, nikitarajia kwamba hatua hii itasaidia kwenye kupatikana muafaka wa kisiasa kwa njia ya amani kuutatua mgogoro uliopo." Ilisema taarifa ya Waziri Mkuu Mykola Azarov iliyochapishwa kwenye mtandao wa serikali.

Azarov amesema serikali yake imefanya kila iwezacho katika kipindi hiki cha mkwamo wa kisiasa ili papatikane suluhisho la amani, na kwamba baraza lake la mawaziri lilikuwa linalazimika kufanya kazi katika mazingira magumu sana.

"Leo, kitu muhimu kabisa ni kulinda umoja na heshima ya Ukraine. Hili ni muhimu zaidi kuliko mipango au matakwa ya mtu binafsi. Na kwa sababu hiyo ndipo nikachukuwa uamuzi huu," imesema taarifa hiyo.

Bunge lakutana kwa dharura

Kujiuzulu kwa Azarov kunakuja huku bunge likiendelea na kikao chake cha dharura mjini Kiev, ambacho kinatazamiwa kujadili njia za kumaliza mgogoro ulioikumba nchi hiyo.

Rais Viktor Yanukovych wa Ukraine.
Rais Viktor Yanukovych wa Ukraine.Picha: AFP/Getty Images

Wabunge walisitisha kwa muda kikao hicho kwa ajili ya kukubaliana ajenda ya leo, dakika chache baada ya wimbo wa taifa na dakika moja ya kuwakumbuka wale waliouawa kwenye mapambano kati ya waandamanaji na polisi mjini Kiev.

Miongoni mwa maamuzi yanayotarajiwa kutoka kwenye kikao hicho ni kuzifuta sheria zinazopiga marufuku maandamano ambauo zilipitishwa na bunge hilo hilo wiki mbili zilizopita.

Bunge pia linatazamiwa kutangaza msamaha kwa waandamanaji wote, kwa masharti kwamba waandamanaji hao waondoke kwenye majengo ya serikali na mitaa wanayoishikilia.

Yanukovych awaalika wapinzani serikalini

Kikao hiki cha bunge kinafuatia mkutano wa masaa manne jioni ya jana kati ya Rais Viktor Yanukovych na viongozi wa waandamanaji, akiwamo waziri wa zamani wa mambo ya nje Arseniy Yatsenyuk, bingwa wa zamani wa masumbwi duniani Vitali Klitschko, na kiongozi wa chama cha siasa za kizalendo, Oleh Tyahnybok.

Kiongozi wa upinzani wa Ukraine, Vitali Klitschko.
Kiongozi wa upinzani wa Ukraine, Vitali Klitschko.Picha: picture-alliance/dpa

Katika mazungumzo hayo, Rais Yanukovych aliwaalika wapinzani hao kuingia kwenye serikali yake, jambo ambalo walilikataa, kwa mujibu wa Waziri wa Sheria, Yelena Lukash.

Waandamanaji wenye hasira wameondoka kwenye jengo la Wizara ya Sheria, lakini wametoa wito ya kuyavamia na kuyakalia majengo yote ya serikali hadi waandamanaji wote waliofungwa jela watakapoachiliwa huru.

Makamu wa Rais wa Marekani, Joe Biden, alizungumza kwa simu na Rais Yanukovych hapo jana, na kumuhakikishia uungaji mkono wa Marekani katika mazungumzo anayofanya na wapinzani kumaliza mkwamo wa kisiasa.

Biden alilaani ghasia zinazofanywa na kila upande wa mgogoro huo, lakini pia akatoa wito kwa serikali kuheshimu imani ya raia kwa Umoja wa Ulaya.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters/AP
Mhariri: Josephat Charo