Yajue mambo ya kushangaza kuhusu miti
Miti hufyonza gesi ya kaboni kutoka angani, inahifadhi wanyamapori na hata kuboresha ustawi wetu wa akili. Lakini unajua kuwa inaweza pia "kuwasiliana” wenyewe kwa wenyewe, na kutuma ishara inapokuwa inashambuliwa?
Kuna spishi 60,000 tofauti za miti
Inakadiriwa kuwa kuna takriban miti trilioni 3 ulimwenguni kote, kulingana na utafiti wa kimataifa ulioongozwa na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Yale. Utafiti huo umejumuisha spishi zipatazo 60,000 za miti, nusu yake zikiwa ni zile zinazopatikana katika nchi moja pekee. Brazil, Colombia na Indonesia ni nchi ambazo kunapatikana idadi kubwa zaidi ya spishi za miti hiyo.
Miti huhama kukimbia mabadiliko ya tabianchi
Miti haiweza kujing’oa na kuhama sehemu ilipo, lakini wingi wake unaweza kupungua kutokana na mabadiliko ya tabianchi. Utafiti uliojumuisha spishi 86 za miti kutoka mwaka 1980 hadi 2015 mashariki mwa Marekani uimegundua kwamba asilimia 73 ya miti ilihamia magharibi mwa nchi ambako kunapatikana mvua kwa wingi. Kwa wastani, miti hiyo inasemekana kuwa ilihama kilomita 16 kila miaka 10.
Miti inaburudisha miji
Mbali na kwamba miti inatupa kivuli, inaweza pia kupunguza joto linapokuwa kali. Inafanya hivyo kwa kunyonya mionzi ya jua na kutoa maji hewani kupitia majani yake. Kawaida sehemu za mijini huwa na joto kali sana wakati wa kiangazi. Lakini utafiti wa mwaka 2019 uliofanywa Marekani umeonyesha kwamba, miti inapofunika asilimia 40 ya mji, wakati wa kiangazi joto linaweza kupungua kwa nyuzi joto 5.
Miti inanyonya vichafuzi vya hewa
Miti huwa inavyonya gesi ya kaboni iliyo hewani na hivyo ina umuhimu sana katika kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Majani pia huchuja gesi zenye sumu zinazochafua hewa kama vile dioksidi ya nitrojeni na dioksidi ya sulfuri. Utafiti wa hivi karibuni uliofanwa Uingereza umegundua kwamba baadhi ya miti ina uwezo wa kupunguza chemcechembe za uchafu hewani kwa hadi asilimia 79.
Miti ina nguvu ya uponyaji
Miti inaweza kupunguza viwango vyetu vya mafadhaiko na kutusaidia kujisikia wenye furaha na afya njema. Chunguzi kadhaa zimeonyesha kwamba kutembea karibu na miti, au hata kutazama tu miti au maua kupitia dirishani, kunaweza kupunguza shinikizo la damu, kuongeza kinga ya mwili, kuboresha usingizi, kupunguza msongo wa mawazo na wasiwasi, na hata kuharakisha mtu kupona baada ya kufanyiwa upasuaji.
Miti inaweza kuwasiliana
Misitu ina mifumo yake ya mawasiliano – ni mtandao unaoruhusu miti kubadilishana virutubisho na kutuma maonyo juu ya ukame au magonjwa. Miti huwasiliana kupitia mitandao ya kuvu kuvu ya kwenye udongo inayojulikana kama mitandao ya mycorrhizal. Utafiti umeonyesha kuwa miti ya paper birch (pichani) na miti ya fir hutumia mfumo huo kupeleka maji, kaboni na virutubisho kutoka mti mmoja hadi mwengine.
Miti hutoa ishara hewani
Miti haiwezi kukimbia pale inapovamiwa na mnyama anayetaka kula majani yake. Lakini inachoweza kufanya ni kutoa kemikali inayosambaa hewani na kuijuulisha miti mingine iliyo karibu kuwa kuna kitisho na ijiandae. Inapopokea ujumbe huo, miti hiyo nayo inazalisha kemikali iliyo na sumu na kwa miti ya acacias (pichani) inayafanya majani yake kuwa machungu.
Miti huomba msaada
Kuna baadhi ya miti inapozingirwa na vimelea kwa mfano miti ya tufaha, nyanya, tango na mimea ya maharagwe ya lima, hutoa kemikali hewani ili kuwatahadharisha wadudu wanaokula vimelea hivyo vilivyoivamia. Lakini utafiti wa Ulaya ulionyesha kuwa miti iliyoathiriwa na viwavi pia hutoa ishara za kemikali ili kuvutia ndege wanaokula viwavi, kwa mfano ndege wa tit (pichani).