Umoja wa Mataifa waonya ongezeko la joto duniani
14 Novemba 2023Katika ripoti iliyotolewa majuma machache kabla ya mazungumzo ya ngazi ya juu ya mabadiliko ya tabia nchi, shirika la Umoja wa Mataifa lenye dhima na mabadiliko ya hali ya lilisema dunia inashindwa kuchukua hatua kwa uharaka wa kutosha kukabiliana na ongezeko la gesi yenye kuchafua mazingira.
Tathmini hiyo inatolewa katika kipindi ambacho ripoti zinaonesha pia kuwa halijoto inaongezeka, na mwaka huu wa 2023 unatarajiwa kuwa wa joto zaidi, katika historia ya binaadamu. Wanasayansi wanasema shinikizo la kukifanya kitisho cha ongezeko la joto duniani halijwahi kuwa jambo la dharura kwa viongozi wa kisiasa, ili waweze kupunguza chanzo cha hali hiyo ambacho ni uzalishaji wa gesi chafu.
Mipango ya mataifa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi haina matumaini.
Umoja wa Mataifa uligundua kuwa mipango ya pamoja ya mabadiliko ya tabia kutoka kwa karibu mataifa 200 itaweka ulimwengu kwenye makadirio ya uzalishaji wa kaboni asilimia mbili kwa 2030 ikiwa ni chini ya viwango vya 2019. Kiwango hicho ni kidogo sana ikiwa ni sawa na kuporomoka kwa asilimia 43 ambapo jopo la wadau wa mazingira la Umoja wa Mataifa-IPCC linasema zinahitajika ili kupunguza ongezeko la joto katika shabaha ya makadirio ya mkataba wa Paris wa nyuzi joto 1.5 tangu zama za kabla ya kiviwanda.
Nikimnukuu hapa Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi Simon Stiell anasema"Kila sehemu ya nyuzi joto ni muhimu, lakini hatujawa vyema. Kwa mkutano wa COP28 ni wakati wetu wa kubadilisha hilo."
Mkutano wa COP28 uwe nusura ya ulimwengu
Aidha ametoa wito kwa mkutano wa mwezi huu wa mabadiliko ya tabia nchi wa mjini Dubai kuonesha juhudi za wazi kwa ulimwengu ambao tayari kwa wakati huu unakumbwa na mafuriko yanayoongezeka, viwango vya joto na vimbunga. Wanasayansi wameonya upo uwezekano wa hatari kushindwa kudhibiti ukomo wa ongezeko la joto duniani la kiasi cha nyuzi joto 1.5 na kunaongoza athari zaidi katika uso wa dunia.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alisema dunia inashindwa kukabiliana na msukosuko wa hali ya hewa na kuonya nchi ambazo hazichukui hatua za kutosha kuepusha janga la mabadiliko ya tabia nchi.
Soma zaidi:Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kufungua pazia leo
Kwa zingatio la mkataba wa Paris wa 2015, mataifa yanapaswa kuwasilisha mipango ya kina ya kupunguza uzalishaji wa gesi chafu, inayojulikana kama Michango Iliyoamuliwa Kitaifa, au kifupi NDC.
Chanzo: AFP