WHO yazindua mchango wa fedha kupambana na COVID-19
10 Februari 2022Mpango huo unaoongozwa na shirika la WHO unanuiwa kuendeleza, kutengeneza, kuagiza na kusambaza vifaa na nyezo za kupambana na janga hilo, zikiwemo chanjo, vipimo, matibabu na vifaa binafsi vya kujilinda. Mfuko wa ACT-A ulizaa mpango wa Covax, ulioandaliwa kuhakikisha nchi masikini zingeweza kufikia chanjo na kubashiri sahihi kwamba mataifa tajiri yangeficha dozi za chanjo. Mpango wa Covax ulitoa dozi yake ya chanjo ya bilioni moja katikati ya mwezi uliopita.
Mfuko wa ACT-A ulihitaji dola bilioni 23.4 kwa mpango wake wa mwezi Oktoba 2021, lakini dola 800 tu zikawa zimekusanywa kama mchango kufikia wakati huo. Mpango huo kwa hiyo unahitaji dola bilioni 16 zitolewe haraka kutoka kwa mataifa tajiri kuziba pengo la fedha lililopo, za zitakazobaki zitatolewa na nchi za kipato cha kati.
Mkurugenzi wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema kuenea kwa kasi kwa kirusi cha Omicron kunaifanya kuwa jambo la dharura kuhakikisha vipimo, matibabu na chanjo zinasambazwa kwa usawa.
"Kama ilivyoainishwa katika mpango wa ufadhili wa kifedha tunaouzindua leo, mfuko maalumu wa kupambana na COVID-19 unahitaji dola bilioni 23 za Marekani kuokoa maisha, kushughulikia kitisho cha Omicron na kuzuia aina hatari za virusi kuzuka. Hiyo inajumuisha fedha za dharura kwa mfuko huo kiwango cha dola bilioni 16 za Marekani."
Ghebreyesus aidha amesema popote tunapoishi COVID-19 bado haijamalizana na sisi. Sayansi imetupa vifaa kupambana na ugonjwa huu na iwapo vitasambazwa kwa usawa kote ulimwenguni tunaweza kuutokomeza kabisa kama janga la dharura la afya la dunia mwaka huu. Asilimia 0.4 pekee kati ya vipimo bilioni 4.7 vya COVID vilivyofanywa ulimwenguni wakati wa janga hili vimetumika katika nchi za kipato cha chini. Asilimia 10 tu ya wakaazi katika nchi hizo wamepata angalau dozi moja ya chanjo.
Shirika la WHO limesema pengo hilo kubwa haligharimu tu maisha na kuathiri uchumi bali pia linatishia kuzuka kwa aina mpya ya virusi ambavyo ni hatari zaidi na vinavyoweza kuharibu ufanisi wa vifaa vya sasa na kurudisha nyuma juhudi za utoaji chanjo kwa miezi mingi katika maeneo ambako watu wengi wamechanjwa.
Guterres asema inawezekana kulitokomeza janga la corona mwaka huu
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo kwamba kulishinda jana hili kunawezekana mwaka huu, lakini tunahitaji kuchukua hatua sasa. Guterres amesema ikiwa tunataka kuhakikisha chanjo inamfikia kila mtu kulitokomeza janga hili, lazima kwanza tuweke usawa katika mfumo mzima wa utoaji chanjo. "Kutokuwepo usawa katika utoaji chanjo ni kushindwa kwa hali ya juu kabisa kwa kizazi chetu, na watu na nchi zinalipa gharama."
Mpango wa ACT-A umekuja na mfumo mpya wa uchangiaji fedha wa haki kuhusu kiwango ambacho kila nchi tajiri inatakiwa kutoa, kwa kuzingatia ukubwa wa uchumi na itakachonufaika nacho kutokana na ukuaji haraka wa uchumi wa dunia.
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, ambaye ni mwenyekiti mwenza wa mfuko maalumu wa kupambana na ugonjwa wa COVID-19, ACT-A amesema kukosekana usawa katika kuzifikia nyenzo za kupambana na COVID-19 kunalirefusha janga hili. Amedokeza kuwa nchi tajiri zimetoa dozi za chanjo za kuokoa maisha mara 14 zaidi na zimefanya vipimo mara 80 zaidi kuliko nchi zenye kipato cha chini. Ramaphosa aidha amesema barani Afrika ni asilimia 8 tu ya watu ambao wamepata dozi kamili za chanjo, na amewatolea wito viongozi wenzake kuonyesha mshikamano zaidi, kutoa michango yao na kusaidia kuyanusuru maisha kutokana na corona.
Naye waziri mkuu wa Norway, Jonas Gahr Store, ambaye pia mwenyekiti mwenza wa mfuko wa ACT-A amesema wanafahamu bila vifaa dhidi ya COVID-19 kuwafikia wote, si ajabu kwamba kasi ya maambukizi itaendelea kubaki juu na wagonjwa, mifumo ya afya na uchumi wa nchi mbalimbali utakabiliwa na mzigo na kudorora. Store amesema aina mpya ya kirusi cha corona huenda kikazuka na kuibua kitisho kwa watu wote ulimwenguni kwa mara nyingine tena, kwa hiyo mpango wa ACT-A ni kwa masilahi ya pamoja kwa nchi zote.
Ramaphosa na mwenyekiti mwenza waziri mkuu wa Norway Jonas Gahr Store wameziandikia nchi 55 tajiri kabisa duniani wakiainisha kiwango wanachotakiwa kutoa na kuzihimiza kulipa. Mpango huo utaitaka Marekani kuchangia kiwango kikubwa zaidi, cha dola bilioni 6. Waziri wa Afya wa Marekani Xavier Becerra, amesema afya ya umma haiishii katika mipaka yao, sote tuko katika kitisho na sote sharti tuchukue hatua kubadili mkondo wa mambo.
ap