1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO: Maambukizi ya Omicron barani Africa yamepungua

Reuben Kyama21 Januari 2022

Kwa mara ya kwanza tangu kutangazwa kwa mlipuko wa virusi vya Omicron, shirika la afya ulimwenguni limesema idadi ya maambukizi mapya ya COVID-19 Africa imepungua na hivyo basi kuleta matumaini miongoni mwa wanasayansi.

https://p.dw.com/p/45s9T
Symbolbild | Impfstoff Corona Omikron Variante
Picha: Fleig/Eibner-Pressefoto/picture alliance

Akihutubia kikao cha waandishi habari kwa njia ya mtandao hapo jana Alhamisi, mkurugenzi wa Shirika la Afya Ulimwenguni kanda ya Afrika, Matshidiso Moeti, amesema ni habari njema kuona visa vya maambukizi ya ugongwa huo vikipungua.

"Nadhani ni bayana na kuna ishara kwamba idadi ya maambukizi kutokana na wimbi la nne la COVID-19 imepungua sio tu nchini Afrika Kusini bali pia kote barani Afrika, kando na maambukizi mapya tunayoyashuhudia kwenye baadhi ya nchi za Afrika kaskazini zinazokabiliwa na majira ya baridi kali".    

Aidha wataalamu kutoka Shirika hilo la Afya Duniani (WHO) wamedokeza kuwa idadi ya vifo kutokana na virusi vya corona barani Afrika imepungua kwa asilimia 8.Wimbi la nne la Covid-19 limefika kileleni barani Afrika-WHO

Hata hivyo, Moeti, aliye raia wa Botswana, ameonya kwamba "japo makali ya wimbi la sasa yanaonekana kufifia, bara la Afrika bado halijaondokana na janga la COVID-19 na hivyo basi kutoa mwito kwa serikali na vyombo vya dola kutolegeza kamba.”

 Matshidiso Rebecca Moeti  World Health Summit  Berlin
Mkurugenzi wa WHO afrika Matshidiso MoetiPicha: DW/Z.Abbany

Ninaamini kwamba haitowezekana kusema ulimwengu mzima umeepukana na janga hili, na kuondoa tahadhari zilizowekwa kujikinga dhidi ya maambukizi ya corona, kama vile kuvaa barakoa, kudumisha umbali wa mita mbili katika sehemu za umma miongoni mwa masharti mengineyo yaliyotolewa na wizara ya afya.

Katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni, utoaji wa chanjo za kupambana na maambukizi ya virusi vya corona umeongezeka kwa kiwango fulani. Phionah Atuhebwe ni afisa wa matibabu kuhusu chanjo dhidi ya corona.

Tuna kipimo cha chanjo milioni 500 zilizowasilishwa na kusambazwa barani Afrika, mchanganyiko wa chanjo kutoka makampuni watengenezaji mbalimbali, na takriban chanjo milioni 330 tayari zimetolewa. Mojawapo ya kizingiti kikuu cha utoaji wa chanjo hiyo imekuwa ni kusitasita kwa baadhi ya watu kukubali kupokea chanjo.

Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni, idadi ya wagonjwa wa COVID-19 barani Afrika imefikia zaidi ya watu milioni 10 ambapo kati ya wagonjwa hao 233,000 wamefariki dunia.