WHO: Hakuna dalili za corona kuisha mwaka huu
2 Machi 2021Shirika la afya duniani WHO linaamini kwamba janga la virusi vya Corona halina uwezekano wa kumalizika katika miezi ya karibuni.
Michael Ryan mkurugenzi wa mpango wa dharura wa shughuli za kiafya katika WHO amesema anadhani ni mapema kufikiria kwamba watalimaliza janga hili kufikia mwishoni mwa mwaka.
Amesema kinachoweza kumalizwa ikiwa ulimwengu utakuwa makini ni idadi ya watu kulazwa hospitali kutokana na virusi hivyo au vifo na matatizo mengine yanayosababshwa na janga hilo.
Nchi za ulimwengu zimetolewa mwito kujiepusha kuondowa haraka shughuli za kudhibiti virusi vya Corona, kutokana na kuwepo chanjo.
Ujerumani kurefusha vizuwizi
Nchini Ujerumani serikali kuu na zile za majimbo zinajiandaa kuongeza muda wa kufunga shughuli mbali mbali hadi Machi 28, kudhibiti maambukizo ya virusi vya Corona.
Vyombo vya habari vimeripoti juu ya uamuzi huo ambapo kansela Angela Merkel na viongozi wa majimbo watakutana kujadili kesho Jumatano.
Merkel na wakuu hao wa serikali za majimbo wanashughulikia mapendekezo ya makubaliano, kuruhusu maduka kufunguliwa tena katika maeneo ambako idadi ya maambukizi ya virusi vya Corona inatajwa kuwa chini kwa kiasi fulani.
Aidha baadhi ya shughuli zinaweza kufunguliwa hata ikiwa kiwango cha maambukizo ni kikubwa, kwa mfano shughuli za biashara ya maua,vitabu na maduka ya vifaa vya bustani.
Kadhalika suala la kuruhusu idadi zaidi ya watu kukutana huenda pia likajadiliwa. Aidha serikali ya Ujerumani inatarajiwa pia kuwatolea mwito wananchi wake kujiepusha na safari za ndani na nje katika kipindi cha msimu wa sikukuu ya pasaka.
Ufaransa yaridhia chanjo ya Astrazeneca
Katika kile kinachoonekana ni mabadiliko ya sera, Ufaransa imeridhia chanjo ya Astra Zeneca kutolewa kwa watu wa umri wa hadi miaka 74.
Waziri wa afya nchini humo Olivier Veran alisema Jumatatu kwamba watu wenye umri wa miaka 65 wenye matatizo ya kiafya wanaweza kupata chanjo ya Astra Zeneca, katika hatua inayoweza kuwagusa zaidi ya watu milioni 2.
Hadi sasa Ufaransa na nchi nyingi za Umoja wa Ulaya ziliruhusu chanjo hiyo kutolewa kwa watu wenye umri mdogo tu, kutokana na ukosefu wa data.
Lakini jana Jumatatu Uingereza ilitowa data zinazoonesha chanjo hiyo ilisaidia kupunguza idadi ya wagonjwa waliolazwa kutokana na Covid 19 kwa zaidi ya asilimia 80.
Chanjo ya Astra Zeneca inatumika sana Uingereza lakini imeshindwa kupeleka chanjo hiyo katika nchi za Ulaya.
Ufaransa imekuwa ikisita kutumia chanjo hiyo ambapo kufikia sasa imetumia dosi 273,000 kati ya dosi 1.7 ilizopokea kufikia mwishoni mwa mwezi Februari kwa mujibu wa takwimu za wizara yake ya afya.
Nchi tatu Afrika zaanza kutoa chanjo
Barani Afrika Nigeria ni nchi ya tatu kupokea chanjo yake ya kwanza ya kuzuia Covid-19 leo iliyotolewa chini ya mpango wa kimataifa wa kugawa chanjo kwa nchi masikini unaitwa Covax.
Nigeria yenye wakaazi milioni 200 imepokea dozi milioni 3.92 za chanjo ya Oxford/AstraZeneca.
Nchi nyingine za Afrika ambazo zimekwishapokea chanjo chini ya mpango huo ni Ghana na Ivory Coast ambazo zimeshaanza kampeini ya kutoa chanjo hiyo.
Mtandao wa kijamii wa Twitta umeanza kufuatilia wanaotoa taarifa za upotoshaji kuhusu chanjo ya kuzuia Covid-19 katika mtandao huo, na umesema utazifuta kwa muda akaunti zitakazochapisha taarifa zisizo sahihi kuhusu chanjo.