WHO: Corona huenda haikuanzia maabara ya Wuhan
10 Februari 2021Wachunguzi wa Shirika la Afya Duniani - WHO waliotafuta chimbuko la virusi vya corona mjini Wuhan wamesema hawakufanikiwa kubaini mnyama aliyeambukiza binadamu na ikiwa kirusi hicho kilianzia mjini huko. Zaidi na saleh Mwanamilongo)
Baada ya wiki nne ya uchunguzi, wataalamu hao wa WHO na wale kutoka China wanashindwa kubaini chanzo cha virusi vya Corona nchini humo. Kwenye mkutano na waandishi habari leo, jopo hilo la wataalamu linasema haiwezekani kuwa virusi hivyo vilitengenezwa kwenye maabara ya kichina. Lakini huenda vikawa vinatokea kwa wanyama na kuwaambukiza binadamu.
''Kirisu hicho kilitokea kwenye nafasi yake ya jadi''
Peter Ben Embarek, mtaalamu wa WHO, na kiongozi wa timu ya uchunguzi amesema kwamba sampuli chungu nzima zilichunguzwa.
'' Shughuli zote zilizofanywa kuhusu virusi na kujaribu kufahamu chanzo chake zinaendelea kuonyesha kwamba kirusi hicho kilitokea kwenye nafasi yake ya jadi,na kama virusi vingine vinavyofanana, ambako ni katika popo ''.
Hata hivyo Embark amesema kunahitajika utafiti maalumu ili kubaini chanzo cha virusi vya Corona. Tangu kuripotiwa visa vya kwanza vya Covid-19 mjini Wuhan, janga hilo tayari limesababisha vifo vya watu zaidi ya milioni 2.3 ulimwenguni kote. Jopo hilo la wataalamu wa Umoja wa Mataifa limeshindwa pia kubaini ikiwa ugonjwa huo ulianza kabla ya Desemba 2019 huko Wuhan.
Ujumbe huo wa kufahamu kuambukizwa kwa virusi kwa binadamu, ulielezewa kuwa muhimu sana ili kufahamu jinsi ya kupambana na janga jingine. Lakini viongozi wa China walisita kuwaruhusu kuingia nchini wataalamu wa afya.
Utafiti unahitaji muda
Mwanzoni shirika la Afya Ulimwenguni, WHO, lilionya kuwa itachukuwa muda ili kubaini chanzo cha janga hili la Corona. Hung Nguyen Viet, mratibu wa mpango wa afya ya binadamu na wanyama kwenye taasisi ya utafiti kuhusu mifugo, mjini Nairobi, amesema utaratibu wa kubaini chanzo cha virusi unahitaji muda na juhudi zaidi.
Huku ziara hiyo ya China ikikamilika, wataalamu wengine wa shirika la WHO wanachunguza ufanisi wa chanjo dhidi ya Codiv-19 ya kampuni ya AstraZeneca ambayo serikali ya Afrika ya Kusini imesema haina nguvu dhidi ya kirusi kipya nchini humo.