Westerwelle awapongeza Wakenya
10 Machi 2013Wakenya wakiendelea kupongezwa kwa uchaguzi wa amani, wametakiwa kuanza hatua ya upatanishi. Hayo yamekuja wakati mpinzani mkuu wa Uhuru Kenyatta, Raila Odinga kuwataka wafuasi wake kuwa watulivu , akijiandaa kuwasilisha malalamiko yake mahakamani kupinga matokeo.
Uhuru alitangazwa mshindi kwa asili mia 50.7 ya kura. Odinga na muungano wake wa CORD wanadai kulikuwa na udanganyifu na kwamba wanaushahidi.
Gazeti la lugha ya Kiingereza The Standard, limesema kauli za upatanishi zilizotolewa na Kenyatta na mgombea wake mwenza William Ruto kutoka muungano wa Jubilee, wakati wa hotuba zao baada ya kutangazwa washindi, bila shaka ni mwanzo mzuri wa kuondoa mgawanyiko wa kikabila katika taifa hilo uliotokana na ushindani wa kisiasa.
Gazeti hilo limesema hayo yamedhihirisha kwamba Kenya imejifunza kutokana na matukio ya 2007 ambapo ghasia zilizofuata zilisababisha zaidi ya watu1,000 kuuawa.
Westerwelle awapongeza Wakenya:
Wakati huo huo Ujerumani Jumapili imewapongeza Wananchi wa Kenya kwa kupiga kura kwa amani .
Katika taarifa yake mjini Berlin, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, alisema kwa hali ya kiutu zaidi na uvumilivu wananchi wa taifa hilo la Afrika Mashariki wametumia haki yao ya kidemokrasia kuamua na wote waliochaguliwa na umma wa Kenya katika nyadhifa mbali mbali wanajukumu la kuwajibika.
Alisema hivi sasa wana kazi ya kukabiliana na changamoto kubwa nchini humo ambayo ni mgawanyiko wa kisiasa , pamoja na kuendelea na mafanikio ya ukuaji wa kiuchumi wa miaka ya hivi karibuni. Westerwelle alisema mustakbali mwema wa Afrika mashariki na kati si jambo la manufaa kwa Kenya pekee bali kwa bara zima la Afrika.
Waziri huyo wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ujerumani akawataka wadau wote nchini Kenya kuheshimu matokeo ya uchaguzi, kutumia busara na wenye malalamiko kuyawasilisha katika vyombo husika vya kisheria.
Westerwelle amesema madai yote ya kuwepo kwa udanganyifu hayana budi kuwa yenye uzito na yashughulikiwe haraka mara baada ya taratibu kufuatwa. Alisema wanamatumaini kwamba wajibu wa Kenya kimataifa utaheshimiwa na kwamba hilo ni pamoja na kushirikiana na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) mjini The Hague.
Mtihani kwa ICC:
Kenyatta na Ruto ni miongoni mwa watu wanne wanaokabiliwa na mashtaka ya kuhusika katika kuandaa machafuko ya baada ya uchaguzi mkuu wa 2007. Kesi dhidi yao zilikuwa zianze kusikilizawa mwezi ujao wa Aprili, lakini sasa ile ya Kenyatta imesongezwa hadi julai wakati kesi dhidi ya Ruto itasikilizwa mwezi Mei.
Wachambuzi wanaashiria kwamba kusikilizawa kwa kesi wakati sasa wanasiasa hao wawili wamechaguliwa kuiongoza Kenya, uatakuwa ni mtihani mkubwa kwa mahakama hiyo ya kimataifa.
Taarifa: Wizara ya Nje - Berlin
Tafsiri: Mohammed Abdul-Rahman, afp
Mhariri: Dahman, Mohamed