1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakenya waombwa kuwa watulivu baada ya Ushindi wa Kenyatta

MjahidA10 Machi 2013

Uingereza imewataka wakenya kuendelea kuwa watulivu na kudumisha amani baada ya Tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC kumtangaza Uhuru Kenyatta kama rais mteule wa Jamuhuri ya Kenya

https://p.dw.com/p/17uSq
Mwenyekiti wa IEBC Issack Hassan
Mwenyekiti wa IEBC Issack HassanPicha: picture alliance/Photoshot

Waziri wa Uingereza anayehusika na maswala ya Afrika Mark Simmonds, akizungumza na chombo cha habari cha AFP ameziomba pande zote mbili muungano wa Cord, wake Raila Odinga na Jubilee unaoongozwa na Uhuru Kenyatta, kuwa wavumilivu na kudumisha amani huku akiwataka wale walioshindwa kukubali au kwenda mahakamani iwapo watakuwa na lawama zozote.

Simmonds amewapongeza wagombea wote lakini pia akasema anaamini mahakama nchini Kenya inaweza kushughulikia lawama zozote zilizojitokeza katika uchaguzi huo.

Baadhi ya wakenya washerehekea ushindi wa Uhuru Kenyatta
Baadhi ya wakenya washerehekea ushindi wa Uhuru KenyattaPicha: Reuters

Uhuru Kenyatta aliepuka kwenda kwenye duru ya pili katika uchaguzi uliofanyika Machi 4 baada ya kujipatia asilimia 50.7 ya kura dhidi ya mpinzani wake Raila Odinga aliyepata asilimia 43.28.

Kulingana na sheria za uchaguzi nchini Kenya, mgombea wa urais ni lazima afikishe zaidi ya asilimia 50 ya kura ili kukwepa kuingia katika duru ya pili, kiwango ambacho Uhuru Kenyatta alipitisha.

Raila Odinga kupinga matokeo ya Uchaguzi

Sasa baada ya Uhuru Kenyatta kutangazwa rasmi rais mteule wa Kenya, mpinzani wake Raila Odinga alisema atakwenda mahakamani kupinga matokeo yaliompa ushindi huo.

Waziri mkuu wa Kenya, Raila Odinga
Waziri mkuu wa Kenya, Raila OdingaPicha: Getty Images/AFP

Odinga amesema matokeo yaliotangazwa na tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC hayakuwa ya haki. Wakati huo huo Raila Odinga aliwaomba wafuasi wake kuwa watulivu.

"Tutaenda mahakamani kupinga matokeo yaliotangazwa na tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC, tunawahimiza wakenya waheshimu sheria na katiba wanayojivunia, na waache mahakama ya juu iamue iwapo matokeo yaliotangazwa na IEBC ni sawa," Alisema Raila Odinga.

IEBC yakanusha visa vya udanganyifu

Matokeo rasmi yalipaswa kutangazwa siku ya Jumatano lakini hitilafu iliyojitokeza katika mfumko wa kielektroniki wa kujumlisha matokeo iliwalazimu maafisa wa IEBC kuanza upya shughuli hiyo kwa kutumia mikono.

Licha ya kulaumiwa kwa kuchelewesha matokeo ya urais, na madai ya visa vya udanganyifu, mwenyekiti wa tume hiyo, Ahmed Issack Hassan, alisema hakuna uwezekano wowote wa matokeo hayo "kuchezewa."

Uhuru Kenyatta ambaye ni mwanae rais wa Kwanza wa Kenya Hayati Mzee Jomo Kenyatta, anakabiliwa na mashtaka katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC, kwa madai ya kuhusika na ghasia za baada ya uchaguzi za mwaka wa 2007.

Rais mteule wa Kenya Uhuru Kenyatta
Rais mteule wa Kenya Uhuru KenyattaPicha: Reuters

Awali Marekani na mataifa mengine ya Magharibi yalisema iwapo Kenyatta ataongoza Kenya kama rais huenda hali hiyo ikatoa changamoto katika masuala ya kidiplomasia kati ya Kenya na jamii ya Kimataifa.

Hata hivyo Rais huyo mteule wa Kenya amesema yuko tayari kufanya kazi na taasisi za kimataifa na kuiomba dunia kuheshimu mamlaka ya Kenya. Uhuru Kenyatta anatarajiwa kuapishwa rasmi tarehe 26 mwezi Machi kama rais wa 4 tangu nchi hiyo ilipopata Uhuru kutoka kwa mkoloni wake Uingereza.

Mwandishi: Amina Abubakar/AP, AFP, dpa, Reuters

Mhariri: Iddi Ssessanga