Kudorora kwa matokeo kwapandisha joto la Wakenya
8 Machi 2013Kundi la kijamii la Concerned Kenyans Initiative limetoa wito kwa Tume ya Huru ya uchaguzi na Mipaka (IEBC) kutangaa matokeo hayo jinsi yalivyo ili Wakenya waweze kurejea katika shughuli zao za kawaida na kumaliza hofu inayopanda kila kukicha.
Hofu hiyo iliongezwa zaidi baada ya mgombea mwenza wa muungano wa CORD, Makamu wa Rais Kalonzo Musyoka, hapo jana kutaka zoezi zima la ujumlishaji kura za urais lisitishwe kwa madai kuwa shughuli hiyo imekumbwa na udanganyifu mkubwa.
“Mfumo wa uwasilishaji matokeo umefeli kabisa na tuna ushahidi wa kutosha kwamba matokeo tunayoyapokea yana dosari”. Musyoka aliwaambia waandishi wa habari.
Kauli hiyo imeliweka taifa katika hali ya taharuki, kwani ilikuja siku moja tu baada ya IEBC kukiri kwamba kumekuwa na hitilafu katika mfumo wake wa kielektroniki wa kujumlisha matokeo na hivyo kurejelea mfumo wa uwasilishaji matokeo wa moja moja kupitia kwa maafisa wa usimamizi wa uchaguzi kutoka majimboni.
Lakini licha ya kulaumiwa kwa kuchelewesha matokeo ya urais, mwenyekiti wa tume hiyo, Ahmed Issack Hassan, anasema hakuna uwezekano wowote wa matokeo hayo "kuchezewa."
“Tume ingependa kuwahakikishia Wakenya kwamba kutokana na juhudi za maafisa wa uchaguzi wanazofanya kuthibitisha matokeo, hakuna nafasi ya matokeo hayo kubadilishwa na ikiwa kuna afisa yeyote atahusika na wizi wa kura, atakabiliwa na sheria yeye binafsi.”
Wakati Wakenya waliokusanyika nje ya ukumbi wa kukusanya matokeo wa Bomas jijini Nairobi wakigandisha macho yao katika ubao wa matokeo, lakini kwa muda wa masaa sita kuanzia saa 8:00 usiku, ubao huo haukutoa mabadiliko yoyote ya kura ya urais.
Jukumu sasa linaachiwa tume ya uchaguzi kuwapa matumaini Wakenya kwa kutangaza matokeo ya urais.
Mwandishi: Alfred Kiti/DW Nairobi
Mhariri: Mohammed Khelef