Waziri mkuu wa Tunisia atishia kujiuzulu
10 Februari 2013Waziri mkuu huyo alitoa wito wa mabadiliko hayo siku ya jumatano, baada ya kuuwawa kwa kiongozi wa upinzani Chokri Belaid, tukio lililosababisha maandamano makubwa ya kupinga mauaji yake.
Chama tawala cha Ennahda nchini Tunisia kinachoongozwa na waziri mkuu Hamadi Jebali, tayari kimepinga pendekezo hilo. Waziri mkuu huyo Hamadi Jebali amesema iwapo hali halisi ya mambo inatazamiwa kubadilika nchini humo, basi ni lazima mawaziri katika serikali wabadilishwe na wale ambao hawana misimamo ya kisiasa. Amesema anadhani anawajibu wa kuiokoa nchi yake inayokabiliwa na kitisho cha kuingia katika ghasia.
Huku hayo yakiarifiwa kumekuwa na maandamano makubwa katika mji mkuu wa Tunisia Tunis ya kuiunga mkono serikali, huku maandamano mengine ya kuipinga serikali na kuishutumu kwa mauaji wa Chokri Belaid yakiendelea. Waandamanaji wanaoipinga serikali walirusha mawe katika ofisi za utawala, na kushambulia vituo vya polisi katika miji kadhaa.
Katika maandamano ya kuiunga mkono serikali, wafuasi wa chama tawala cha Ennahda waliandamana wakiilani Ufaransa mkoloni wao wa zamani kwa kuingilia siasa za Tunisia. Wiki iliopita waziri wa ndani wa Ufaransa Manuel Valls, alilaani mauaji ya Belaid akiyaita mashambulizi dhidi ya hadhi ya mageuzi ya nchi hiyo.
Kulingaana na wizara ya ndani ya Tunisia takriban watu 230 walio na umri wa miaka 16 hadi 25, wamekamatwa tangu siku ya Ijumaa, wakati Chokri Belaid alipozikwa. Jana Jumamosi(09.02.2013) ndio iliokuwa siku ya tatu ya mfululizo wa ghasia katika taifa hilo la Afrika kaskazini lililomuondoa rais wake wa miaka mingi Zine El Zine El Abidine Ben Ali, mnamo januari mwaka 2011. Maandamano ya nchini Tunisia ndio yaliochochea vuguvugu la maandamano katika mataifa mengine ya Kiarabu katika eneo la mashariki ya kati.
Chokri Belaid kiongozi wa upinzani nchini humo, na pia mwanaharakati wa haki za binaadamu alipigwa risasi na watu wasiojulikana nje ya nyumba yake siku ya Jumatano wiki iliopita. Mauaji hayo yamezidi kuongeza hali ya wasiwasi nchini humo ambako kipindi cha mpito kutoka kwa udikteta hadi katika njia ya demokrasia kimekuwa kikikumbwa na maswala tofauti ikiwemo ya kidini, kisiasa na hata kiuchumi.
Mkewe Belaid aomba Ulinzi wa familia yake
Huku hayo yakiarifiwa mkewe Marehemu Chokri Belaid ameiomba wizara ya mambo ya ndani nchini humo kutoa ulinzi kwake na watoto wake. Basma Belaid amesema iwapo kitu chochote kitamtokea yeye au binti zake ataishitaki rasmi wizara hiyo kwa kutompa ulinzi.
Belaid aliyezikwa siku ya Ijumaa aliuwawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana nje ya nyumba yake. Familia yake imekishutumu chama tawala cha Ennahda kwa kuhusika na mauaji hayo lakini chama hicho kimekanusha vikali.
Katika taarifa yake mkuu wa chama cha Ennahda Rached al-Ghannouchi, amesema wanaanzisha mipango ya kuwapeleka mahakamani wale wote wanaodai kuwa chama hicho kimehusika na mauaji ya Belaid. Ghannouchi amesema, wanasiasa na hata waandishi habari watashitakiwa iwapo watapatikana wakieneza habari hizo za uwongo juu ya mauaji ya Belaid.
Kipindi cha mpito nchini Tunisia kimesifika kuwa tulivu kuliko ilivyofanyika, Libya na Misri lakini kwa sasa kuna hofu taifa hilo huenda likatumbukia katika ghasia.
Mwandishi Amina Abubakar/AP/Reuters
Mhariri Sekione Kitojo