1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri mkuu wa Tunisia kuunda serikali mpya

MjahidA7 Februari 2013

Waziri mkuu wa Tunisia ameahidi kuunda serikali ya wataalamu kwa ajili ya uchaguzi mpya, baada ya mauaji ya kiongozi wa upinzani Shoukri Belaid kuzua maandamano makubwa na shutma nyingi kutolewa kwa serikali tawala.

https://p.dw.com/p/17a54
Waziri Mkuu wa Tunisia Hamadi Jebali
Waziri Mkuu wa Tunisia Hamadi JebaliPicha: AFP/Getty Images

Waandamanaji waliojawa na hasira waliandamana na kushambuliana na vikosi vya serikali nchini humo, huku makundi manne ya upinziani likiwemo kundi la marehemu Shoukri Belaid la muungano wa vyama vya kisiasa unaoitwa Popular Front wakitoa wito kujitoa bungeni. Kulingana na wizara ya ndani, polisi mmoja aliuwawa baada ya kupigwa mawe kifuani kwenye maandamano hayo ya jana.

Kwa sasa waziri mkuu anayetokea chama cha waislamu Hamadi Jebali amesema ataunda utawala mpya usioegemea upande wowote wa kisiasa ili kushughulikia maswala ya nchi kabla ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika katika muda mfupi.

Ghasia Tunisia
Ghasia TunisiaPicha: AFP/Getty Images

Hata hivyo Jebali amesema atalivunja bunge na kuunda utawala wa muungano wa kitaifa, kufuatia mauaji ya kiongozi huyo wa upinzani lakini haikujulikana moja kwa moja ni lini hasaa atalivunja bunge hilo. Wakati huo huo Chama cha Ennahda kimetupilia mbali wazo la waziri mkuu la kulivunja bunge hilo.

Rais wa Tunisia alaani mauaji ya Shoukri

Kwa upande wake rais wa Tunisia Moncef Marzouki amelaani vikali mauaji ya Belaid aliyepigwa risasi na kuuwawa nje ya nyumba yake jana.

"Haya ni mauaji ya kinyama dhidhi ya mwanasiasa niliyemfhamau kwa muda mrefu, ambaye ni rafiki yangu kwa miaka mingi, ningependa kuzungumzia katika bunge kuwa ni kitisho" Alisema rais Marzouki

Belaid alikuwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya Tunisia. Hata hivyo mkuu wa chama tawala cha Ennahda Rached Ghannouchi kilichoshutumiwa kwa mauaji hayo na familia ya Belaid kimekanusha kuhusika na mauaji hayo.

Rais wa Tunisia Moncef Marzouki
Rais wa Tunisia Moncef MarzoukiPicha: dapd

Wiki iliopita marehemu Shoukri Belaid alikishutumu chama cha Ennahda kwa kutuma mamluki kuwashambulia wafuasi wa chama chake huku akionya kuwa waasi hao wamekodiwa ili kuwahangaisha wananchi wa Tunisia na kuisukuma nchi hiyo katika ghasia.

Huku hayo yakijiri makundi ya Upinzani nchini humo yanamnyooshea kidole cha lawama waziri wa ndani Ali Laraydeh kutoka chama tawala cha Ennahda kwa mauaji ya Belaid na kutaka afutwe kazi mara moja, kwa kuwa kulingana na makundi hayo Ali Laraydeh, alifahamu vitisho vya kuuwawa alivyokuwa akipokea Belaid lakini hakuna chochote kilichofanywa na wizara hiyo.

Mwili wa Shoukri Belaid ukiingizwa katika gari la wagonjwa
Mwili wa Shoukri Belaid ukiingizwa katika gari la wagonjwaPicha: REUTERS

Marekani pamoja na nchi kadhaa za kigeni zimelaani mauaji hayo huku shirika la kutetea haki za binaadamu la human rights watch likiuhimiza utawala nchini Tunisia kuhakikisha wale waliohusika wanakabiliwa na mkono wa sheria.

Kiongozi huyo wa upinzani Shoukri Belaid anatarajiwa kuzikwa kesho baada ya sala ya Ijumaa.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman