Waziri mkuu wa Tunisia ajiuzulu
20 Februari 2013Baada ya kujiuzulu kwa Hamadi Jebali hapo jana, hii leo rais wa nchi hiyo ya Tunisia Moncef Marzouki anatarajiwa kufanya mazungumzo na Kiongozi wa chama tawala cha Ennahda Rached Ghannouchi, huku nchi hiyo ikizidi kuyumbayumba kisiasa. Viongozi hao wawili wanatarajiwa kumchagua waziri mkuu mpya. Nchi hiyo haina uwezo wa kuunda serikali mpya bila ya chama cha Ennahda kuridhia kwa kuwa ndio walio na viti vingi bungeni.
Awali Jebali, ambaye ameitumikia nchi yake kama waziri mkuu kwa muda wa miezi 15 alitishia kujiuzulu iwapo pendekezo lake la kuunda serikali ya wataalamu, kusuluhisha migogoro ya nchi hiyo na kuiongoza Tunisia katika uchaguzi wa mapema halitazingatiwa.
Badala yake chama chake cha Ennahda ndicho kilichokuwa cha kwanza kupinga pendekezo hilo, na kuiweka nchi hiyo katika hali mbaya kisiasa, kidemokrasia na hata kuididimiza zaidi katika mdororo wa kiuchumi. wanasiasa kadhaa wa kidini waliunga mkono mpango wa Jebali lakini chama chake cha Ennahda kilipinga kwa kuwa na hofu ya kutengwa na vyama vyengine.
"Niliapa kuwa iwapo mpango wangu hautafanikiwa, nitajiuzulu, na nimeshafanya hivyo," Alisema Jebali alipokuwa katika mkutano na vyombo vya habari hapo jana, baada ya kukutana na rais Moncef Marzouki.
Lawama za mauaj kwa chama tawala
Ghasia za kisiasa nchini humo tangu kufanyika vuguvugu la maandamano mwaka 2011, lililomuondoa madarakani rais wa zamani Zine El Abidine Ben Ali, zilianza baada ya kuuwawa kwa kiongozi wa upinzani Chokri Belaid. Belaid aliuwawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana nje ya nyumba yake takriban wiki mbili zilizopita.
Hakuna mtu aliyekiri kuhusika na mauaji hayo ingawa wengi nchini humo wanailaumu serikali ya Jebali kwa kushindwa kupambana na wanasiasa walio na itikadi kali za kidini wanaotishia uthabiti wa nchi hiyo. Hata hivyo Familia ya Belaid ilitoa lawama za moja kwa moja kwa chama cha Ennahda kwa kuhusika na mauaji hayo hatua ambayo chama hicho kilikanusha vikali.
Ghasia zinazoendelea Tunisia zimetatiza mipango ya kufufua uchumi wa nchi hiyo baada ya kushuka wakati wa kuangushwa utawala wa rais wa zamani Ben Ali. Tunisia imekuwa ikijadiliana na shirika la kimataifa la fedha duniani IMF kupata mkopo wa dola bilioni 1.78 ili kuokoa uchumi wake.
Mwandishi Amina Abubakar/AP/Reuters
Mhariri Yusuf Saumu