1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri mkuu wa China atambelea Berlin

27 Mei 2013

Ziara ya waziri mkuu wa China mjini Berlin, mtego wa ndege zisizokuwa na rubani, kampeni ya uchaguzi mkuu na fainali ya kombe la vilabu bingwa barani Ulaya Champions League ndizo mada zilizohanikiza magazetini.

https://p.dw.com/p/18eWe
Waziri mkuu wa China Li Keqiang(kushoto) na kanswla Angela Merkel katika mkutano na waandishi habari mjini BerlinPicha: Reuters

Tuanzie lakini Berlin na ziara ya waziri mkuu wa jamhuri ya umma wa China Li Keqiang. Umoja wa Ulaya unaikosoa China miongoni mwa mengineyo kuhusu bei ya chini kabisa ya mitambo ya kunasia nguvu za jua. Hata hivyo gazeti la "Stuttgarter Zeitung" linaandika:Kansela Angela Merkel anataka kujitahidi kuuepusha mvutano huo usizidi makali.Kansela Merkel sawa na waziri wa uchumi Philipp Rösler ameelezea nia ya kusaka maridhiano ambayo ni kwa masilahi ya Ujerumani. China sio tu inazidi kujipatia umuhimu barani Ulaya kwasababu ya matatizo ya kiuchumi katika nchi nyingi za kanda ya Euro bali pia akiba kubwa ya sarafu ya nchi hiyo tajiri inazifanya nchi za kanda ya Euro zisifanye mchezo. Hata hivyo hiyo isiwe sababu ya kutozungumziwa masuala yanayozusha mivutano. Umoja wa Ulaya una kila sababu ya kukosoa mtindo wa kibiashara wa China. Na miaka ya nyuma imedhihirisha pia uwezekano upo wa kuepusha mvutano usizidi makali.

Mtego wa ndege bila ya rubani

Verteidigungsminister Thomas de Maizière mit Soldaten der deutschen Mali-Truppe
Waziri wa ulinzi Thomas de Maizière akiwatembelea wanajeshi wa Ujerumani walioko Dakar Senegal kwa lengo la kuwapatia mafunzo wanajeshi wa MaliPicha: picture-alliance/dpa

Kadhia ya ndege za upelelezi zisizokuwa na rubani inazidi kumkaba waziri wa ulinzi Thomas de Maizière.Kila kukicha mepya yanafichuliwa.Gazeti la "Westdeutsche Zeitung" linaandika:"Kwa mara ya kwanza katika maisha yake ya kisiasa, waziri wa ulinzi amenasa mtegoni.Alikuwa na malengo chungu nzima alipofikiria kutumia ndege za upelelezi zinazoruka bila ya rubani,ili kulinda maisha ya wanajeshi. Lakini katika utekelezaji wake uzembe mkubwa umetokea na ambao de Maizière atabidi awajibike pengine kisiasa. Bado anajivunia imani ya kansela, lakini wanasiasa wengine wameshajionea kwa haraka vipi msimamo wa kansela unabadilika katika kadhia kama hii. Na katika kipindi kama hiki cha karibu na uchaguzi mkuu ndio kabisa."

Walinzi wa mazingira wapwaya

Homa ya uchaguzi mkuu inazidi kupanda miezi chini ya mitano kabla ya uchaguzi wenyewe kuitishwa. Gazeti la Stuttgarter Nachrichten" linaandika jinsi mpango wa walinzi wa mazingira Die Grüne wa kuanzisha kodi ya juu ya mapato kwa wanaopokea mishahara mikubwa mikubwa, unavyowageukia wenyewe. Gazeti linaendelea kuandika:" Kodi ya mapato inayopendekezwa na walinzi wa mazingira imegubika yote yale yaliyopendekezwa na chama cha SPD. Ndio maana watu hawazungumzii tena kuhusu SPD bali walinzi wa mazingira die Grüne. Lakini walinzi wa mazingira wameshindwa kutambua kwamba mipango yao haipigiwi makofi peke yake. Mipango ya kuwalipisha walio nazo,pengine haichomi sana. Lakini tangazo la kuzidishiwa kodi wote wenye kulipwa mishahara mikubwa,linawachoma wengi tu ambao walitaka kuwapigia kura walinzi wa mazingira.Linaziumiza familia,ambazo ingawa wana mishahara mikubwa, lakini si tajiri na wala hawajisikii kama ni watu wanaofaidika na mgogoro wa fedha. Mjadala uliozuka katika jamii kuhusu mipango ya walinzi wa mazingira kuwatoza kodi kubwa ya mapato wenye kupokea mishahara mikubwa, umeshaanza kuleta madhara:imani ya wapiga kura kwa chama cha die Grüne imeanza kupungua."

Ndoto ya FC Bayern haiko mbali kukamilika

UEFA Champions League Finale (Borussia Dortmund vs. Bayern München)
Kocha wa Bayern Munich,Jupp Heynckes akishangiriwa na wanasoka wake katika uwanja wa michezo wa Wembley mjini LondonPicha: picture-alliance/dpa

Na hatimae fainali ya kombe la vilabu bingwa barani Ulaya-Champions League.Gazeti la "Donaukurier" linaandika:"FC.Bayern-nyota ya kusini,ndivyo inavyotajwa katika wimbo wa timu hiyo ya mjini Munich. Na walioutunga hawajakosea. Angalau safari hii. Nyota ya kusini ina ng'ara kuliko wakati wowote ule mwengine. Ushindi katika uwanja wa Wembley sio tu kilele cha msimu wa kusisimua, bali pia jaza ya juhudi zilizoanzishwa miaka mingi iliyopita. Jupp Heynckes-nani asiyemuonea kijicho? - Jaza hiyo itakamilika pengine June mosi ijayo mjini Berlin."

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Khelef