1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Li Keqiang azuru Ujerumani kuimarisha ushirikiano

27 Mei 2013

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ameahidi kutumia ushawishi wa kiuchumi wa nchi yake, kuuzuia Umoja wa Ulaya usiziwekee vikwazo vya ushuru baadhi ya bidhaa zinazoagizwa kutoka China, ili kuepusha vita vya kibiashara.

https://p.dw.com/p/18ePx
Waziri Mkuu wa China Li Keqiang akiwa na Angela Merkel mjini Berlin
Waziri Mkuu wa China Li Keqiang akiwa na Angela Merkel mjini BerlinPicha: Reuters

Kansela Merkel aliyasema hayo katika mkutano wa waandishi wa habari mjini Berlin jana jioni, akiwa na waziri mkuu wa China, Li Keqiang, ambaye yuko ziarani nchini Ujerumani.

''Ujerumani itapigia debe mazungumzo ya kina kati ya Umoja wa Ulaya na China, kutafuta suluhisho katika tofauti zao za kibiashara haraka iwezekanavyo.'' ameyasema Kansela Merkel, ambaye nchi yake ndiyo yenye uchumi imara zaidi barani Ulaya, akiwa na mgeni wake, waziri mkuu wa China, Li Keqiang, mjini Berlin.

Halmashauri ya Umoja wa Ulaya wenye nchi 27 wanachama inaishutumu China kupunguza bei za bidhaa zake kama vile paneli za nishati ya jua na vifaa vya mawasiliano, kwa makusudi ya kulifurika soko la Ulaya na kukwamisha ushindani, hali ambayo inayaumiza makampuni ya Ulaya.

Ulaya huishutumu China kurundika paneli za bei nafuu kwenye soko lake
Ulaya huishutumu China kurundika paneli za bei nafuu kwenye soko lakePicha: STR/AFP/Getty Images

Ujumbe usio sahihi

Umoja huo umependekeza paneli kutoka China ziwekewe ushuru wa kiwango cha asilimia 47, na unaendelea kutafakari hatua za kuchukua dhidi ya vifaa vya mawasiliano. Waziri Mkuu Li amepinga vikali hatua hizo, na kusema zinatuma ujumbe usio sahihi.

''Maoni yetu kuhusu kuweka vizingiti vya masoko, ni kuwa hatua hiyo inawaharibia wengine bila kuleta manufaa kwa aliyeichukua. Hususan ukizingatia mazingira ya utandawazi, hatua hizo hazitaleta mafanikio yoyote. Hatua hizo ni za kutiliwa mashaka, hasa wakati huu ambapo mgogoro wa kifedha haujapatiwa ufumbuzi, na bado uchumi wa dunia haujaweza kusimama kwa miguu miwili.'' Amesema Li.

Umoja wa Ulaya ni mshirika wa pili kwa ukubwa kwa China kibiashara baada ya Marekani, na thamani ya biashara kati ya pande hizo mbili ilifikia euro bilioni 430 mwaka 2012. Biashara ya paneli za nishati ya jua ilikuwa asilimia 7 ya bidhaa kutoka China zilizouzwa barani Ulaya. Umoja wa Ulaya unatarajiwa kufanya maamuzi juu ya uchunguzi kuhusu bidhaa zinazorundikwa kwenye soko lake, baada ya mashauriano na wadau wote ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Ujerumani yaahidi kukinga kifua

Kansela Merkel amesema pande mbili zinapaswa kuiepusha hali hiyo. ''Ujerumani itafanya juhudi kuhakikisha tatizo hili linapatiwa ufumbuzi haraka kama inavyowezekana, kwa sababu hatuamini kwamba vikwazo vya ushuru vitaleta tija kubwa. Kwa sababu hiyo hatuna budi kufanya kazi kubwa mnamo miezi sita ijayo, na Ujerumani itahakikisha kwamba mazungumzo yanapiga hatua.''

Merkel na Li wakikagua gwaride la heshima
Merkel na Li wakikagua gwaride la heshimaPicha: AFP/Getty Images

Ujerumani ni nchi pekee ya Umoja wa Ulaya aliyoitembele Li Keqiang, katika ziara hii ambayo ni ya kwanza nje ya nchi tangu alipochaguliwa kuchukuwa wadhifa wa waziri mkuu wa China mwezi Machi mwaka huu, na hilo limechukuliwa kama hatua ya makusudi kutaka kutumia nguvu za Ujerumani kiuchumi kushawishi maamuzi ya Umoja wa Ulaya.

Makampuni makubwa ya kijerumani yanapinga vikwazo kwa China, yakiohofia kuwa kushamiri kwa mzozo wa kibiashara kwaweza kuudhuru uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi hizo mbili.

Wakati wa ziara yake waziri mkuu wa China na kansela Merkel wamefanya mazungumzo na wanafunzi kutoka pande mbili, na kusaini mikataba kadhaa ya ushirikiano wa kiuchumi. Leo hii, waziri mkuu Li Keqiang atakutana na viongozi wa makampuni mbali mbali, na pia atafanya mazungumzo na mpinzani wa Angela Merkel katika uchaguzi wa mwezi Septemba, Peer Steinbrueck.

Mwandishi: Daniel Gakuba/APE/AFPE

Mhariri:Josephat Charo