1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMali

Waziri Mkuu Mali afutwa kazi kwa kuukosoa utawala wa kijeshi

21 Novemba 2024

Mkuu wa kijeshi wa Mali Kanali Assimi Goita amemfuta kazi Waziri Mkuu wa kiraia Choguel Kokalla Maiga na serikali yake. Hii ni siku chache tu baada ya Maiga kufanya ukosoaji wa nadra wa watawala wa kijeshi.

https://p.dw.com/p/4nEB4
Choguel Kokalla Maiga
Choguel Maiga alionekana kutengwa katika wadhifa wake wa uwaziri mkuu.Picha: Israel Matene/REUTERS

Amri iliyotolewa na Kanali Goita na kusomwa kwenye televisheni ya taifa ORTM imesema majukumu ya waziri mkuu na maafisa wa serikali yamesitishwa. Maiga, ambaye aliteuliwa na jeshi mwaka wa 2021, Jumamosi iliyopita alilaani hadharani ukosefu wa uwazi kuhusiana na kukamilika kwa kipindi cha mpito kuelekea utawala wa kiraia. Alisema mkanganyiko huo unaweza kusababisha matatizo makubwa na kuhatarisha nchi kurudi nyuma.

Soma pia: Raia wa Mali wakabiliana na maisha magumu tangu mapinduzi

Maiga alionekana kutengwa katika wadhifa wake wa uwaziri mkuu. Kutimuliwa kwake kunasababisha sintofahamu zaidi katika utawala ambao tayari una matatizo.

Soma pia: Utawala wa kijeshi Mali wajadili mikakati ya kudhibiti hali ya usalama

Baada ya mapinduzi ya 2020 na 2021, jeshi liliahidi Juni 2022 kuandaa uchaguzi na kukabidhi madaraka kwa raia ifikapo Machi 2024, lakini baadae likaahirisha uchaguzi hadi wakati usiojulikana.