Waziri Mkuu Ahmed awaongoza wanajeshi vitani
24 Novemba 2021Haya yanafanyika wakati jamii ya kimataifa ikiwa imeingia hofu kuhusiana na mzozo huo unaozidi na wakati wapiganaji wa Tigray wakidai kuukaribia Mji Mkuu Addis Ababa huku raia wengi wa kigeni wakiambiwa waondoke nchini humo.
Taarifa za vyombo vya habari nchini humo zinasema naibu Waziri Mkuu Demeke Mekonne Hassen sasa ndiye atakayechukua jukumu la shughuli za kawaida za serikali kufuatia kuondoka kwa Waziri Mkuu Ahmed.
Msemaji wa serikali Legesse Tulu amezungumzia kwa kina kuhusiana na kuhamishwa huko kwa baadhi ya madaraka kwa muda katika afisi ya naibu waziri mkuu.
TPLF lauteka mji karibu na Addis Ababa
Haya yanafanyika wakati Umoja wa Mataifa ukiwa unasema umeamrisha kuondolewa nchini humo kwa wafanyakazi wake wa kimataifa na familia zao huku Ufaransa ikiwa nchi ya hivi karibuni ya Magharibi kuwaambia raia wake waondoke katika nchi hiyo iliyozongwa na mzozo kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.
Stephane Dujarric ni msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres.
"Kutokana na hali ya ukosefu wa usalama nchini humo na kwa ajili ya kuchukua tahadhari tu, Umoja wa Mataifa umeamua kupunguza nyayo zake Ethiopia na kuwahamisha kwa muda wafanyakazi wake. Ni muhimu kufahamu kwamba baadhi ya wafanyakazi watasalia ili kutimiza majukumu yetu muhimu," alisema Dujarric.
Kundi la Ukombozi wa Watu wa Tigray TPLF wiki hii lilidai kwamba limeuteka mji mmoja ulioko kilomita 220 hivi kutoka Mji Mkuu Addis ingawa madai yanayotolewa katika uwanja wa mapambano nchini Ethiopia si rahisi kuyathibitisha kutokana na ukosefu wa mawasiliano.
Hapo Jumatatu Waziri Mkuu Abiy Ahmed aliapa atawaongoza wanajeshi wake katika mapambano katika kile ambacho serikali imekiita "vita vinavyoendelea" katika nchi ya pili yenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika.
Kuna matumaini katika kupatikana mwafaka katika mazungumzo
Mambo haya yanatilia mashaka matumaini ya kufikishwa mwisho kwa mapigano hayo ambayo yamezua hofu kwamba huenda yakaenea katika eneo zima la Pembe ya Afrika.
Lakini mjumbe wa Marekani Jeffrey Feltman anasema anaona hatua zikipigwa kuelekea kusitishwa kwa mapigano katika mazungumzo kati ya pande mbili zinazozozana nchini Ethiopia ingawa anahofia kwamba mapambano ya kijeshi huenda yakalemaza juhudi hizo.
Masuala yanayotarajiwa kuletwa kwenye meza ya mazungumzo na ingawa masuala hayo yanafanana, tofauti zinaibuka katika suala lipi kulipa kipau mbele katika mazungumzo hayo.
Kama ishara ya upinzani kutoka kwa vikosi vya Tigray, kulitolewa taarifa na afisi ya mambo ya nje ya Tigray iliyosema "hatua yoyote ya amani ambayo lengo lake ni kumlinda Abiy Ahmed asiangushwe, haitopewa sikio na TPLF."
Lakini mjumbe wa Marekani Feltman amesema vikosi vya Tigray ni sharti visitishe kuusogelea mji mkuu wa Addis Ababa kwa kuwa matakwa yao yataongezeka kadri wanavyozidi kuukaribia mji huo.
Vyanzo: Reuters/AFPE/APE