1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Abiy asema yuko tayari kuongoza mapambano dhidi ya TPLF

23 Novemba 2021

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amesema yuko tayari kuelekea kwenye uwanja wa mapambano kuongoza wanajeshi wa serikali wanaopambana na wapiganaji waasi.

https://p.dw.com/p/43M57
Äthiopien | Premierminister Abiy Ahmed Ali
Picha: Minasse Wondimu Hailu/AA/picture alliance

Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa Twitter, Waziri Mkuu Abiy Ahmed ambaye ni mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel ya mwaka 2019 amesema yuko tayari kuwa katika mstari wa mbele kuongoza mapambano dhidi ya waasi.

Ameandika, "Wale wanaotaka kuwa miongoni mwa watoto wa Ethiopia ambao watasifiwa na historia, amkeni kwa ajili ya kuitetea nchi yenu leo. Tukutane katika mstari wa mbele." 

Soma pia: Ethiopia: Daniel Bekele, mtetezi wa haki au kibaraka wa serikali?

Kauli ya Abiy ambaye amewahi kuwa mwanajeshi, ameitoa wakati wapiganaji wa kundi la waasi la TPLF wakiripotiwa kuukaribia mji mkuu Addis Ababa, na kudaiwa kuuteka mji wa Shewa Robit, uliopo kilomita 220 kaskazini mashariki mwa Addis Ababa.

Akijibu kauli hiyo, msemaji wa kundi la TPLF Getachew Reda ameandika kwenye mtandao wa Twitter kuwa wapiganaji wa kundi hilo kamwe hawatorudi nyuma katika harakati zao.

TPLF yasema haitorudi nyuma katika harakati zao

Äthiopien Mekele | Pro-TPLF Rebellen
Wapiganaji wanaounga mkono waasi wa TPLFPicha: YASUYOSHI CHIBA/AFP

Taarifa ya Waziri Mkuu huyo pia imedai Mataifa ya Magharibi yanaipiga vita serikali ya Addis Ababa, kauli hiyo ikiwa ya hivi karibuni katika kile serikali inachokielezea kuwa ni uingiliaji wa jamii ya kimataifa.

Muda mfupi tu baada ya taarifa ya Abiy, afisa wa ngazi ya juu katika wizara ya mambo ya nje wa Marekani aliwaambia waandishi habari kuwa Marekani bado inaamini kuwepo fursa ndogo ya kupatanisha pande zinazohasimiana.

Jana Jumatatu, kamati kuu ya chama tawala cha Prosperity ilikutana ili kujadili juu ya vita hivyo vilivyodumu kwa mwaka mmoja sasa. Baada ya mkutano huo, Waziri wa Ulinzi Abraham Belay aliliambia shirika la habari la serikali kuwa, vikosi vya usalama vitachukua mkondo tofauti bila ya kutoa maelezo zaidi.

Soma pia: Marekani yasema TPLF kuilenga Addis Ababa ni kitisho kikubwa

Belay amesema lazima waikomeshe hujuma inayofanyiwa watu wao na wapiganaji waasi wa TPLF.

Hofu ya waasi kuingia mji mkuu Addis Ababa umezishurutisha nchi kadhaa ikiwemo Marekani na Uingereza kuwaondoa baadhi ya wafanyikazi wake katika balozi zao. Hata hivyo serikali imepuuza ripoti kuwa waasi wanaendelea kupata nguvu kwa kusema ripoti hizo zimetiwa chumvi.

Inakadiriwa kuwa, maelfu ya watu wameuawa katika vita hivyo kati ya vikosi vya usalama vya serikali na wapiganaji waasi kutoka jimbo la Kaskazini la Tigray. Marekani pamoja na mataifa mengine ya Magharibi yametahadharisha kuwa mzozo huo unatishia kuliyumbisha eneo la Pembe ya Afrika.