1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroSudan

Watumishi wa umma Sudan wapambana na hali ngumu

12 Julai 2023

Mapigano yanayoendelea Sudan kati ya majenerali mawili wanaozozana yamesababisha vifo na hasara kubwa. Kwa wale waliobaki nchini humo sasa wanapitia hali ngumu ya kimaisha.

https://p.dw.com/p/4TjT3
Sudan Ärzte ohne Grenzen
Picha: ASHRAF SHAZLY/AFP

Imad Mohammed ni mwalimu wa shule ya umma nchini Sudan. Alikuwa amefanya kazi kwa miaka 32 wakati vita vilizuka karibu miezi mitatu iliyopita na kuiharibu nchi yake pamoja na kipato chake. Anasema kwa sasa wanapata mlo mmoja tu kwa siku katika familia yake ya watu watano. Mwalimu huyo kutoka jimbo la Al-Jazirah, ambalo mpaka sasa limenusurika mapigano makali lakini bado linakabiliwa na uhaba mkubwa, anasema hawajui hali hii itaendelea mpaka lini.

Soma pia: Sudan yakataa kushiriki mkutano wa IGAD na Kenya

Kama tu ilivyo kwa watumishi wengine wa umma, Mohammed hajalipwa mshahara tangu jeshi la Sudan na vikosi vya wanamgambo wa RSF walipoanza kupigana.

Kombobild Abdul Fattah Al-Burhan und Mohamed Hamdan Dagalo
majenerali wa kijeshi Sudan Abdul Fattah Al-Burhan na Mohamed Hamdan Dagalo wanagombania madarakaPicha: Bandar Algaloud/Mahmoud Hjaj/AA/picture alliance

Wakati miripuko ya kwanza iliitikisa Khartoum mnamo Aprili 15, mabenki mjini humo yaliifunga milango yao, na matawi kote nchini yamekumbwa na matatizo tangu hapo kutoa huduma kwa sababu yametenganishwa na makao makuu katika mji mkuu. Tangu wakati huo, mishahara pekee ya serikali ambayo imelipwa ni ya jeshi.

Karibu wafanyakazi milioni moja wa sekta ya umma wanalazimika kuishi kwa kutegeme akiba zao au mitandao ya misaada ya kijamii. Ammar Youssef, mkuu wa Kamati ya Walimu nchini Sudan anasema wanachopitia walimu na familia zao, katika sekta za umma na binafsi, ni janga.

Soma pia: Umoja wa Mataifa: Sudan ipo hatarini kuingia 'vita kamili'

Mapigano hayo tayari yamewauwa watu 3,000 na kusababisha wengine milioni tatu kuyakimbia makwao. Zaidi ya watu milioni 1.5 wamekimbia Khartoum pekee, wakitumia fedha zozote walizokuwa nazo wakati mapigano yalipoanza, ili kuepuka mashambulizi ya angani, makombora na mapigano ya mitaano ambayo yameugeuza mji mkuu huo kuwa uwanja wa vita.

Lakini wengine ambao hawakubahatika kuwa na fedha kiasi au akiba yoyote walishindwa kuondoka. Wamekwama mjini humo, wasiweze kulipia gharama kubwa za usafiri kwa sababu bei za mafuta zimeongezeka mara ishirini Zaidi.

Nchi kadhaa zaondoa raia wake Sudan

Youssef anasema kuwa elimu ya umma pekee huajiri zaidi ya watu 300,000, ambao tayari walikuwa wanalipwa mshahara duni kabla ya vita, akiongeza kuwa wizara ya elimu haipatikani tangu vita vilipozuka. Anasema wale ambao hawauliwi kwa risasi watakufa kwa njaa.

Huku bei za vyakula zikiendelea kupanda, nazo bidhaa za msingi zikiendelea kupungua na mishahara kusitishwa, Zaidi ya nusu ya wakaazi milioni 48 nchini humo wanahitaji msaada, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa. Unaiorodhesha Sudan kama moja ya maeneo yenye tahadhari kubwa ya uhaba wa chakula na kuonya kuhusu haja ya kuchukuliwa hatua ya dharura kutoka kwa jamii ya kimataifa.

Benki kuu ilitangaza mapema Julai kuwa matawi yake katika majimbo mengi ya Sudan yameanza tena kutoa huduma, jambo lililoongeza matumaini ya baadhi ya watu. Lakini kwa mujibu wa mchumi Mohamed al-Nayer, hali katika miezi michache ijayo itakuwa mbaya hata Zaidi. Hata kabla ya vita, uchumi wa Sudan ulikuwa umeathirika na kiwango kikubwa cha mfumko wa bei.

Vyama kadhaa vya wafanyakazi ambavyo vimeshindwa kupata jibu kutoka kwa serikali ya Khartoum, vimeungana na kuonya kuwa watafanya mgomo, ambao huenda ukaongeza mivutano hata zaidi nchini Sudan.

Muungano wa wawakilishi wa madaktari, walimu, wahandishi, wahadhiri wa vyuo vikuu na waandishi habari wametangaza kuwa watachukua hatua dhabiti ikiwa hawatolipwa mishahara.

afp