Umoja wa Mataifa: Sudan ipo hatarini kuingia 'vita kamili'
10 Julai 2023Umoja huo umetoa tahadhari hiyo baada ya mashambulizi ya angani siku ya Jumapili katika eneo la makaazi ya watu kusababisha vifo vya zaidi ya watu 20.
Wizara ya afya ya Sudan iliripoti kuwa watu 22 waliuawa na wengi walijeruhiwa. Kulingana na wizara hiyo, mashambulizi hayo yalifanyika siku ya Jumamosi katika mji wa Omdurman, hasa mtaa wa Dar al-Salam, inayomaanisha nyumba ya amani katika lugha ya Kiarabu.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, kupitia taarifa iliyotolewa na naibu wake, Farhan Haq, alilaani shambulizi hilo la mjini Omdurman.
Soma pia: Misri kuwa mwenyeji wa mkutano wa kutafuta amani Sudan
Haq ameendelea kusema kwenye taarifa hiyo kwamba Guterres ana wasiwasi kuhusu vita vinavyoendelea Sudan kati ya vikosi vyenye silaha, ambavyo vimeisogeza nchi hiyo katika ukingo wa kutumbukia kwenye vita kamili vya wenyewe kwa wenyewe, hali ambayo inaweza kuyumbisha utulivu wa kanda hiyo nzima.
Baada ya takribani miezi mitatu ya vita kati ya majenerali wawili, shambulizi hilo kutoka angani ndilo la hivi karibu zaidi kuibua ghadhabu.
Miili iliyokatikatika mitaani
Kanda ya video iliyochapishwa na wizara ya afya katika ukurasa wake wa Facebook ilionesha miili iliyokatika vipande vipande ikiwa imefunikwa ardhini, baada ya shambulizi la angani.
Kikosi chenye nguvu cha wanamgambo RSF kinachopambana dhidi ya jeshi la taifa, kilidai shambulizi hilo la angani liliua watu 31.
Wakaazi waliozungumza na shirika la habari la AFP, pia walikiri kutokea shambulizi la angani.
Lakini hapo jana vikosi vya jeshi vilitoa taarifa na kueleza kuwa, kikosi chao cha jeshi la angani hakikushughulikia mashambulizi yoyote ya adui yaliyolenga eneo la Omdurman.
Mashuhuda waliripoti pia kwamba mashambulizi zaidi ya angani yalifanyika Jumapili karibu na ikulu ya rais mjini Khartoum na pia mjini Omdurman. Wameongeza pia kuwa kulikuwa na mapigano makali ya risasi na zana nyingine nzito kusini mwa mji huo.
Makabila ya Darfur yanaweza kubadili mwelekeo wa vita Sudan
Hayo yakijiri, mashuhuda wamesema raia wameanza kuchimba makaburi kuwazika waliouawa kwenye shambulizi la Jumamosi.
Tangu vita vilipoanza, miili mingi imeachwa tu ikioza mitaani hasa katika miji ya Khartoum na Darfur ambayo imeshuhudia mapigano makali.
Marufuku ya usafiri wa angani Sudan yarefushwa
Mamlaka ya usafiri wa angani imerefusha muda wa kufungwa kwa anga ya Sudan hadi Julai 31, isipokuwa safari ambazo zimeidhinishwa za misaada ya kiutu na uokozi. Hayo ni kulingana na usimamizi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Khartoum.
Takriban watu 3,000 wameshauawa kwenye machafuko hayo tangu yaanze mwezi Aprili. Aidha manusura wamekuwa wakiripoti kukumbana na manyanyaso ya kingono. Mashuhuda pia wamesema yapo mashambulizi yanayolenga makabila.
Makabiliano yapamba moto Sudan bila kuwepo dalili za maridhiano
Kumekuwa na uporaji mwingi. Umoja wa Mataifa umeonya huenda uhalifu wa kibinadamu umefanyika katika jimbo la Darfur lililoko magharibi ya nchi hiyo.
Shirika la Kimataifa la Uhamiaji linasema karibu watu milioni tatu wamekimbia nchi yao Sudan kufuatia machafuko hayo, wakiwemo watu 700,000 ambao wamekimbilia nchi nyingine jirani.
(Chanzo: AFPE)