Watu wanne wafariki kufuatia maporomoko ya udongo Kenya
9 Aprili 2024Kwa wiki ya tatu sasa,mvua kubwa zimekuwa zikishuhudiwa sehemu mbalimbali ya taifa huku uharibifu mkubwa ukiendelea kuripotiwa.
Jimbo la Narok limekuwa la hivi punde kuripoti hasara kutokana na mvua. Watu wanne wa familia moja kutoka Kijiji cha Torokiat wamefariki baada ya nyumba yao kuporomokewa na udongo.
Mvua hizo kadhalika zimesababisha mamlaka ya kitaifa inayosimamia barabara nchini KeNHA ,kufunga baadhi ya barabara za humu nchini ikiwemo ile ya North Horr kuelekea Kalacha baada ya mafuriko kuharibu barabara hiyo.
Mvua yasababisha maafa zaidi Kenya
Katika jimbo la Kisumu,angalau familia mia tatu kutoka eneo bunge la Nyando zimeachwa bila makazi kufuatia mvua hizo. Wakaazi wakiilalamikia serikali ya kaunti hiyo kwa kushindwa kushughulikia tatizo la mafuriko kila mara mvua inaponyesha.
Nairobi pia imeathirika kwa mvua hiyo kubwa
Jimbo la Nairobi pia limekuwa likishuhudia mvua kubwa,wakaazi wakimtaka Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja kuwajibika. Wanailaumu serikali ya kaunti hiyo kwa kushindwa kujenga mabomba ya kupitisha maji ambayo ndiyo chanzo cha mafuriko katika mitaa mbalimbali.
Hayo yakijiri,basi la abiria lililokuwa likitoka Garissa kuelekea Nairobi lilisombwa na mafuriko katika Daraja la Areli japo abiria wote waliondoka bila majeraha. Kamanda wa Polisi wa jimbo la Tana River Ali Ndiema amethibitisha kuwa,juhudi za uokozi zinaendelea.
Ikumbukwe, idara ya utabiri wa hali ya anga,imetangaza kuendelea kushuhudiwa kwa mvua kubwa haswa maeneo ya pwani,kati na magharibi mwa kenya kwa wiki hii. Hadi sasa,hakuna takwimu iliyotolewa na serikali au shirika la msalaba mwekundu kuhusu idadi kamili ya maafa kutokana na mvua ya sasa.
Michael Kwena, DW Marsabit