Mvua yasababisha maafa zaidi Kenya
29 Aprili 2020Baadhi ya maziwa na mito pia imefurika hivi kuzua hofu ya mkurupuko wa magonjwa. Wataalam wanaiambatanisha hali hiyo na uharibifu wa mazingira.
Kwa kuyatizama kutoka mbali Ziwa Nakuru na Ziwa Naivasha yanaonekana kuongezeka kwa upana, athari ya mvua kubwa inayonyesha ikijidhihirisha. Ziwa Victoria na mito Tana na Nzoia ni miongoni mwa maeneo yaliyofurika na kusababisha uharibifu wa makaazi, miundo mbinu na mashamba katika maeneo tofauti nchini Kenya yakiwemo Kisumu, Busia, Bomet, Kericho, Narok, Naivasha na Garissa.
Mafuriko hayo yamewasababisha maelfu ya watu kuyahama makaazi yao. Shirika la msalaba mwekundu nchini limeeleza kuwa watu 29 wamekufa kufuatia maporomoko ya ardhi. Jackson Raini, ambaye ni mtaalam wa maswala ya mazingira amesema uharibifu wa misitu unachangia pakubwa maziwa kujaa maji.
"Maziwa haya yako kwenye sehemu ya chini zaidi ya vyanzo vya maji na ukumbuke kwamba vyanzo hivi vimeharibiwa sana. Kati ya asilimia 50 ya misitu tuliyokuwa nayo mwaka 2000, sasa tuna asilimia 7 tu ya misitu, kwa sababu ya watu kupewa makaazi katika maeneo haya. Zamani misitu hii ingeyakusanya maji wakati wa mvua nyingi na kuyaachilia pole pole, lakini sasa mvua inaponyesha maji hayo yanashuka kwa haraka mitoni hadi kwenye maziwa.”
Wanawake, watoto, wazee na wagonjwa ndio walio hatarini zaidi, wahanga hawa sasa wakiwa wamechukua hifadhi katika shule mbalimbali. Hali hii ya mafuriko inazua hofu ya mkurupuko wa magonjwa kama vile kipindupindu.
Sospeter Ojamong, Gavana wa Busia anasema serikali imeanza kutoa msaada wa dawa za kuwakinga na magonjwa hayo ikiwa ni pamoja na kuwapa msaada wa vyakula, blanketi na mahitaji mengine muhimu.
Eric Ogada, mkaazi wa Nakuru anaikosoa serikali kwa kutoshughulikia janga hili kwa wakati ufaao akisema suluhu la kudumu linahitajika kuyanusuru maisha ya Wakenya wengi.
Tahadhari ya Idara ya utabiri wa hali ya hewa nchini kwamba baadhi ya mito ingevunja kingo zake, iliwafanya baadhi ya watu kuyahama makaazi yao ambao bado wangali wanasubiri msaada wa serikali.