1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu milioni 50 wanaswa katika 'utumwa mamboleo': Ripoti

24 Mei 2023

Korea Kaskazini, Eritrea na Mauritania zinaongoza kwa kukithiri kwa utumwa Mamboleo ulimwenguni. Faharasa ya Utumwa Ulimwenguni ya mwaka wa 2023 inabainisha hali kuwa mbaya tangu utafiti wa mwisho miaka mitano kabla

https://p.dw.com/p/4RjWd
Zahl der Opfer von moderner Sklaverei stark gestiegen
Picha: Mey Dudin/dpa/picture alliance

Ripoti iliyochapishwa leo Jumatano inasema kiasi ya watu milioni 50 waliishi katika kile ilichosema ni "mazingira ya utumwa mamboleo” katika mwaka wa 2021, ikiwa ni ongezeko la watu milioni 10 kutoka mwaka wa 2016, wakati tatizo hilo lilipimwa mara ya mwisho.

Soma pia: Utumwa Afrika bado haujatokomezwa

Idadi hiyo inajumuisha watu milioni 28 walioko katika kazi za kulazimishwa na milioni 22 wanaoshi katika ndoa za kulazimishwa.

Zahl der Opfer von moderner Sklaverei stark gestiegen
Korea Kaskazini ambayo inatawaliwa kimabavu ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa utumwa mamboleoPicha: Dita Alangkara/AP/dpa/picture alliance

Uchunguzi huo umesema kuwa hali inazidi kuwa mbaya zaidi wakati kukishuhudiwa ongezeko la mizozo ya kivita, uharibifu mkubwa wa kimazingira na athari za janga la virusi vya corona, miongoni mwa sababu nyingine.

Ripoti hiyo iliyotayarishwa na shirika la hisani la haki za binaadamu la Walk Free, inafafanua utumwa wa kisasa kama unaojumuisha kazi za kulazimishwa, ndoa za kulazimishwa, utumwa wa madeni, biashara ya kulazimishwa ya ngono, usafirishaji haramu wa binadamu, vitendo vinavyofanana na utumwa, na uuzaji wa Watoto na kuwatumia vibaya.

Soma pia: Nchi za ulimwengu zatakiwa zichukue hatua kupambana na maovu ya utumwa,

Msingi muhimu wa utumwa unahusu "kuondolewa kimfumo kwa uhuru wa mtu” – kutoka haki ya kukubali au kukataa au kukataa kazi hadi uhuru wa kuamua kama, lini na nani wa kufunga ndoa naye.

Kwa kigezo hiki, Korea Kaskazini iliyojitenga na ya kimabavu ndiyo ina kiwango kikubwa cha kuenea kwa utumwa wa kisasa (104.6 kwa kila watu 1,000), kulingana na ripoti hiyo. Inafuatwa na Eritrea (90.3) na Mauritania (32), ambayo mwaka 1981 ilikuwa nchi ya mwisho duniani kuharamisha utumwa wa kurithi.

Waafrika wauzwa kwa mnada kama watumwa huko Libya

Nchi kumi zenye utumwa mamboleo uliokithiri zina sifa zinazofanana, ikiwemo "ulinzi mdogo wa uhuru wa raia na haki za binaadamu.” Nyingi ya nchi hizo zipo katika maeneo "tete” yanayokumbwa na mizozo au ukosefu wa utulivu wa kisiasa, au ni nyumbani kwa idadi kubwa ya "watu wanaoishi katika mazingira magumu” kama vile wakimbizi au wafanyakazi wahamiaji.

Katika nafasi kumo za kwanza ulimwenguni ni Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu na Kuwait, ambako haki za wafanyakazi wahamiaji zinadhibitiwa na mfumo wa ufadhili wa "kafala.”

Nchi nyingine katika kumi bora ni Uturuki, "ambayo inawahifadhi mamilioni ya wakimbizi kutoka Syria,” Tajikistan, Urusi na Afghanistan.

Wakati kazi za kulazimishwa ni kitu cha kawaida katika nchi za kipato cha chini, inaunganishwa pakubwa na mahitaji ya nchi za kipato cha juu, imesema ripoti hiyo.

Ripoti hiyo imesema nchi za G20 – zinazoundwa na Umoja wa Ulaya na madola 19 makubwa kiuchumi – kwa sasa zinaagiza bidhaa za thamani ya dola bilioni 468 ambazo zipo katika hatari ya kuzalishwa kwa nguvu kazi ya kulazimishwa, kutoka dola bilioni 354 katika ripoti ya awali.

Bidhaa za kieletroniki zinasalia kuwa zenye thamani ya juu zilizo hatarini, zikifuatiwa na nguo, mafuta ya mawese na paneli za jua, ikiwa ni dalili ya kuwepo na mahitaji makubwa ya bidhaa za nishati mbadala.

afp