Utumwa Afrika bado haujatokomezwa
2 Desemba 2021Kauli mbiu hii inaashiria vuguvugu la ulimwengu kukomesha mateso na uonevu ambao mizizi yake imejikita katika biashara ya utumwa na utumwa wenyewe, kwa lengo la kuhamasisha juu ya umuhimu wa kuelemisha kuhusu historia ya biahara ya utumwa na utumwa ili kuleta utambulisho wa athari za utumwa katika ulimwengu wa sasa. Lengo pia ni kutafuta mikakati ya kushughulikia athari za muda mrefu zilizosababishwa na utumwa kama vile ubaguzi, upendeleo na vitendo vya ukiukwaji wa haki.
Cheickna Diarra anatokea kijiji cha Baramabougou katika eneo la Keyes nchini Mali. Huko utumwa wa kurithi umeenea. Diarra pia alilazimika kutii amri ya wale aliowaita kuwa mabwana wake na waliotendea maovu na ukatili. Katika maojiano na DW Diarra amesema mnamo 2019 aliponea chupu chupu kifo baada ya kumtembelea rafiki.
"Nilipokuwa njiani kurejea nyumbani, takriban vijana 20 kutoka kijijini walinizuia njia bila kuniuliza natokea wapi na nilichokuwa nikikifanya hapo. Ghafla walianza kunipiga na vijiti na kunitandika mpaka nikaanguka chini na kupoteza fahamu."
Alifanikiwa kujinusuru kutokana na vilio vya jamaa zake waliowafahamisha wakaazi wengine wa kijiji hicho ambao walikuja kumsaidia.
Malalamiko hayashughulikiwi
"Hatujayalima mashamba yetu tangu 2018. Wale wanaodai ni mabwana wetu wametupiga marufuku kwenda madukani au mashambani au kuondoka kijijini"
Hatimaye Diarra aliwasilisha malalamiko dhidi ya watu wasiojulikana ambao walimnyanyasa. Hakufanikiwa. Akakimbilia mji mkuu Bamako, na sasa anaishi katika kambi ya watu waliolazimika kuyakimbia makazi yao yenye jumla ya watu 130, wengi wao walikata tamaa baada ya malalamiko yao kutokushughulikiwa.
Shirika la Temedt linapigania kupigwa marufuku utumwa wa kistaarabu au wa kurithi nchini Mali. Raichatou Walet Altanata ndiye makamu rais wa shirika hilo. "Kama shirika la kutetea haki za binadamu tumekuwa tukilaani utaratibu huu tangu 2006. Lakini hatujawahi kuwa kesi hata moja iliyofika mahakamani. Mamlaka mara zote hupata sababu. za kuzuia"
Katika mahojiano na DW Altanata amekosoa kwamba wakati mwingine huchukuliwa kama kitendo cha udhalilishaji, mara nyingine kama kosa la uhalifu, lakini sababu hasa ya kimsingi ambayo ni utumwa, haizingatiwi kabisa.
Tabia hii ni kinyume na sheria na sjheria za kimataifa ambazo Mali iliridhiria katika kupambana na utumwa. Lakini pia inakinzana na sheria msingi ya nchi hiyo inayosema utu wa mtu unatakiwa kuheshimiwa na haupaswi kuingiliwa.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Anti Slavery limeandika kwamba utaratibu wa kurithi hadhi ya utumwa bado unapatikana katika ukanda wote wa Sahel, ikiwemo Mauritania, Niger, Mali, Chad na Sudan. Kwa mfano linasema watu wanalazimika kulisha mifugo, kufanya kazi mashambani au majumbani mwa mabwana wao bila malipo katika jamii nyingi za kiafrika, na pia kuna mfumo wa kitamaduni ambapo watu wanafahamika kama kizazi cha watumwa au wamiliki au mabwana wa watumwa. Mauritania ndiyo iliyokuwa nchi ya mwisho barani Afrika kupiga marufuku utumwa mnamo 1981, lakini hali halisi ni tofauti nchini humo.
Utumwa mamboleo: Watu wanakabiliwa na shinikizo
Mnamo Desemba 2, 1949, Umoja wa Mataifa uliridhia mkataba wa kudhibiti usafirishaji wa watu na unyanyasaji wa wengine. Wakati huo huo siku hiyo ilitangazwa kama siku ya kimatiafa ya kupiga marufuku utumwa. Zaidi ya miaka 70 baadaya, mkataba huo umepoteza umuhimu wake.
"Hatua kubwa zimepigwa katika kufahamu utumwa mamboleo na ushawishi ulio nyuma yake, lakini bado tuna safari ndefu kama tunataka kweli kuutokomeza kabisa," anasema Jasmine O'Connor, mwenyekiti wa shirika la kimataifa la kupambana na utumwa Anti Slavery International katika mahojiano na DW.
"Mamilioni ya watu kote ulimwenguni wanaishi katika utumwa na shinikizo linaloongezeka huwafanya wengine wengi kukabiliwa na kitisho zaidi cha tambo za wafanyabiashara haramu ya kusafirisha binadamu."
Kwa mujibu wa shirika la kazi la kimataifa ILO, zaidi ya watu milioni 40 duniani kote ni wahanga wa utumwa mamboleo - asilimia 25 kati ya walioathiriwa ni watoto. O'Connor anataraji takwimu kuhusu watoto wanaotumikishwa zitaongezeka na zitatolewa hivi karibuni.
Ingawa utumwa mamboleo haujafafanuliwa maana yake kisheria, unatumiwa kama mwavuli wa vitendo kama vile utumikishaji wa kutumia nguvu, vifungo vya madeni, ndoa za lazima, usafirishaji wa binadamu na kuwaandikisha watoto kwa nguvu jeshini. Watu barani Afrika wameathirika kwa kiwango kikubwa, kufuatiwa barani Asia na eneo la Pasifiki.
Ajira ya watoto imeongezeka baada ya miaka 20
Kwa mujibu wa shirika la ILO watu milioni 15.4 ulimwenguni kote wameathiriwa na ndoa za lazima. Watu milioni 24.9 wako katika ajira za lazima, kati yao, wawili kati ya watatu wanatumikishwa katika sekta ya kibinafsi kama vile wafanyakazi wa majumbani, katika maeneo ya ujenzi au kilimo. Shirika la ILO linasema watu milioni 4.8 wananyanyaswa kingono na milioni nne wanalazimishwa kufanya kazi na mamlaka za serikali. Takwimu hizi ni za tangu mwaka 2016, na hakuna zozote zilizopatikana hivi karibuni.
Janga na mabadiliko ya tabia nchi yachochea unyanyasaji
Jasmine O'Connor, mwenyekiti wa shirika la kimataifa la kupambana na utumwa Anti Slavery International amesema katika mahojiano na DW kwamba hatua kubwa zimepigwa katika kufahamu utumwa mamboleo na ushawishi ulio nyuma yake, lakini bado tuna safari ndefu kama tunataka kweli kuutokomeza kabisa.
O'Connor anatoa wito hatua zaidi madhubuti zichukuliwe, sheria muafaka zitekelezwe, uchunguzi ufanywe na hatua za kuepusha vitendo vya utumwa ziwekwe katika kila nchi ili kutokomeza kabisa utumwa. Amesema mataifa yaliyostawi kiviwanda duniani G7 yameutambua utumwa kama suala lenye umuhimu mkubwa.