Watu 44 wauwawa Nigeria
24 Agosti 2013Taarifa zinasema unyama huo umefanyika katika kijiji cha Demba kilichopo karibu na mji wa Baga kaskazini mwa jimbo la Borno, sehemu iliyokuwa ngome ya kundi la Boko Haram kabla ya kusambaratishwa na jeshi katikati ya mwezi Mei. Kitendo hicho kiliwafanya wanamgambo wa kundi hilo kukimbilia mafichoni au kuvuka mpaka kuingia nchi jirani ya Cameroon.
Kuchelewa kwa taarifa za mauwaji
Shambuzili limeelezwa kufanyaka Jumatatu lakini taarifa zake zimeibuka hivi karibuni kutokana na eneo hilo kuwa katika maeneo ya vijijini sana na kwamba mawasiliano ya simu yalikatwa na serikali kwa lengo la kuvuruga operesheni za Boko Haram.
Kundi hilo linataka kuwepo kwa sheria za Kiislamu katika eneo la pamoja na vikundi vingine vya Waislamu ambavyo vilikuwa kitisho kikubwa cha usalama wa Nigeria.
Baadhi ya raia wamechinjwa
Mmoja kati ya wafanyakazi wa huduma ya dharura katika eneo hilo aliyezungumza na shirika la habari la reuters kwa masharti ya kutotajwa jina lake kwa kuhofia usalama wake, alisema walichoma moto nyumba, kupiga risasi watu, na kuwachinja watu. Maafisa wa usalama katika maeneo hayo wamethibitisha kutokea vifo hivyo.
Shumbulio hilo limefanyika siku ambayo serikali pia ilitangaza kuwa mmoja kati ya viongozi muhimu wa Boko Haram, Aboubakar Sheka atakuwa ameuwawa kati ya Julai 25 na Agosti 4, kutoka na jeraha alililolipata baada ya kutokea mapigano kati ya kundi hilo na vikosi vya usalama vya serikali.
Tangazo la Mauwaji na kifo cha kiongozi wa Boko Haram
Madai ya kifo cha kiongozi huyo yametajwa kulipunguza nguvu kundi hilo lakini pia uwezo wa kutekeleza operesheni zake unaonekana kupungua tangu rais wa Nigeria Goodluck Jonathan kutangaza hali ya hatari huko kaskazini mwa Nigeria, katika majimbo matatu yaliyoathirika vibaya zaidi na kuanzisha rasmi mpango maalumu wa kulisambaratisha mwezi Mei mwaka huu.
Baga ni mji ulioshuhudia mapigano yaliyojumuisha wanajeshi wa Nigeria, Chad na Niger na wanamgambo wa Kiislamu mwezi Aprili ambayo yalisababisha vifo vya idadi kubwa ya watu. Jeshi lilisema watu 37 waliuwawa lakini viongozi wa mji huo walisema kaasi watu 185, wengi wao wakiwa raia wasio na hatia waliuwawa katika vurugu hizo.
Jeshi lilisema Boko Haram waliwauwa watu wengine 20 katika mji huo mwezi uliopita. Nigeria taifa lenye zaidi ya watu milioni 160 barani Afrika limekuwa na migogoro ya kidini ambayo kwa kiasi kikubwa inasababishwa na Waislamu kwa upande wa kaskazini na Wakristo kusini.
Mwandishi: Sudi Mnette RTR
Mhariri: Sekione Kitojo