Waandishi wa kimataifa wapewa tuzo ya DW
15 Agosti 2013Tangu mwaka 1975 tuzo hiyo imekuwa ikitolewa kwa waandishi wa habari wanaofanya kazi bora ya kuripoti juu ya haki za binaadamu na maendeleo. Kwa mara ya kwanza mwaka huu, tuzo hiyo imetolewa kwa waandiishi wa habari wa kimataifa kwa ushirikiano wa DW na wizara ya ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo ya hapa Ujerumani. Zilitolewa tuzo saba, sita kwa waandishi kutoka kanda mbali mbali za ulimwengu, na tuzo moja maalumu kwa wapiga picha wa Kiafrika.
Waziri wa maendeleo wa Ujerumani, Dirk Niebel, alisisitiza umuhimu wa waandishi wa habari kwa ajili ya maendeleo ya jamii. Kwa sababu hiyo, tuzo inawaenzi wale wasiokubali kunyang'anywa haki yao ya kutoa maoni, alisema Niebel na kuongezea kwamba lengo ni kuwapongeza waandishi wa habari wanaoripoti juu ya maendeleo na hali ya haki za binaadamu katika nchi zao kwa ujasiri mkubwa na mara nyingi katika mazingira magumu.
Naye mkurugenzi wa DW, Erik Bettermann, aliongezea, "Tuzo hii ni ya kuwatia moyo wengine waingilie kati na kupaza sauti zao. Tunataka wafahamu kwamba hawako pekee yao!"
"Penye nia pana elimu"
Tuzo ya eneo la Amerika ya Kusini ilikwenda kwa watengenezaji wa tovuti inayoelezea kisa cha watu waliotoweka nchini Colombia. Majaji waliwasifu washindi kwa kutumia ubunifu wao na kudhihirisha namna ambavyo visa vinaweza kuelezwa kwa njia tofauti katika mtandao wa intaneti. Mshindi mwingine aliyeamua kuelezea ripoti yake mtandaoni ni mjerumani Uwe Martin. Yeye amefanya uchunguzi kuhusu uzalishaji wa pamba na namna unavyoharibu maisha ya wakulima wa zao hilo.
Kulikuwa pia na tuzo maalumu, ambapo umma ndio uliochagua nani awe mshindi. Tuzo hiyo ilitolewa kwa mpiga picha Oluyinka Ezekiel Adeparusi kutoka Nigeria. Picha yake inaonyesha watoto katika eneo la mabanda la Makoko, mjini Lagos. Watoto hao wamekaa katika boti na wako njiani kuelekea nyumbani wakitokea shuleni. Kichwa cha picha hiyo kinasema: "Penye nia pana elimu."
Majaji waliwasifu washindi kutoka India na Liberia kwa kuweka uwiano kati ya kuguswa na kisa kinachoripotiwa na kwa upande mwingine kuweka umbali fulani kati yao na kisa wanachokizungumzia. Wade Williams kutoka Liberia alisema "Aliye mwandishi wa habari ana kalamu mkononi. Kalamu hiyo inaweza kutoa sauti kwa wale wanaoihitaji."
Mwandishi: Ralf Witzler
Tafsiri: Elizabeth Shoo
Mhariri: Josephat Charo