Watoto wanasaidia kusafisha mazingira
8 Agosti 2006Kwa mfano nchini Ufilipino,familia hukusanya mifuko mitupu ya vinywaji,huisafisha na baadae huishona kuwa mikoba,ambayo ina soko kubwa katika jiji la New York nchini Marekani.Sasa wanafunzi wa chuo kikuu cha Trier kutoka Ujerumani wameanzisha mradi kama huo katika mji mkuu wa Kenya,Nairobi.
Nchini Ujerumani kila taka hutiwa katika mapipa maalum;kwa mfano karatasi,chupa na plastiki hutengwa mbali mbali.Lakini katika maeneo ya madongo poromoka katika nchi za Afrika Mashariki mambo ni tofauti kabisa.Si kwamba taka hazitengwi tu,bali mara nyingi taka hizo wala hazikusanywi na hutupwa njiani tu.
Sasa wanafunzi wa chuo kikuu cha Trier wanajaribu kuubadili mtindo huo.Kuambatana na mradi ulioanzishwa Nairobi,watoto hukusanya mifuko ya plastiki iliyotupwa ovyo njiani na baadae hupata pesa kwa kuiuza mifuko hiyo.Mtu atadhani kuwa ni shida kupata pesa kutokana na taka,lakini mradi huo unakwenda vizuri katika kitongoji cha Mathare cha jiji la Nairobi.Watoto na vijana wanaweza kuuza kilo moja ya mifuko ya plastiki kwa bei ya shilingi tano za Kenya.Kwa maoni ya watoto inafaa kufikiria mazingira.Ujumbe wa watoto wa kitongoji cha Matahre ni huu:
“Safisha mazingira yetu,taka ni pesa,haraka kusanyeni pesa.”
Katika kitongoji cha Mathare,mifuko ya plastiki ipo kila mahala na mara nyingi huziba mifereji na taka hurundikana.Taka hizo sasa hukusanywa na watoto hao pamoja na wanafunzi wa chuo kikuu cha Trier.Mwanafunzi mmojawapo ni Michael Öhmann. Anasema kuwa kabla ya hivi sasa mifuko hiyo ya plastiki,haikuwa na thamani.Lakini mradi uliyoanzishwa Nairobi umefungua soko la kufanya biashara ya mifuko ya taka iliyokusanywa.
Watoto wanatambua kuwa ulinzi wa mazingira unaleta faida.Siku hizi watoto hao hawatupi ovyo mifuko ya plastiki kwani pesa wanazopata huwasaidia.Kwa mfano wanatumia pesa hizo kununua chakula shuleni.
Bila shaka watoto hao wataendelea kuyalinda mazingira yao huku wanafunzi wa chuo kikuu cha Trier wakifurahi kuona kuwa tatizo la taka za mifuko ya plastiki limegeuzwa kuwa biashara kubwa.