1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watoto wa Gaddafi kusimamishwa kizimbani

14 Aprili 2014

Wana wawili wa kiongozi wa zamani wa Libya Muamar Gaddafi wanafikishwa mahakamani leo, katika kesi ambayo vile vile inawahusisha maafisa wengine wapatao 30 wa enzi za utawala wa Gaddafi.

https://p.dw.com/p/1BhR0
Mmoja wa watakaofikishwa kizimbani, Saif al-Islam
Mmoja wa watakaofikishwa kizimbani, Saif al-IslamPicha: dapd

Watoto hao wawili wa Gaddafi wanaopandishwa kizimbani leo ni Saadi Gaddafi na Saif al-Islam, na wote wanakabiliwa na tuhuma za ufisadi pamoja na uhalifu wa kivita. Tuhuma nyingine wanazokabiliwa nazo ni za mauaji, utekaji nyara, kuhamasisha ubakaji, na matendo mengine yaliyotishia usalama wa taifa.

Jumuiya ya kimataifa inaifuatilia kwa makini kesi yao ambayo pia inawashirikisha maafisa wengine zaidi ya 30 waliohudumu katika utawala wa miongo minne wa Muamar Gaddafi. Miongoni mwa maafisa hao wengine ni aliyekuwa mkuu wa shughuli za kijasusi Abdullah Senussi, na waziri mkuu wa mwisho wa utawala wa Gaddafi, Al-Baghdadi al-Mahmudi.

Kipimo cha demokrasia

Namna itakavyoendeshwa itatoa sura ya maendeleo yaliyofikiwa katika kuweka utawala wa sheria na demokrasia nchini Libya, baada ya mapinduzi ya mwaka 2011 ambayo yaliambatana na ghasia.

Mkuu wa zamani wa upelelezi wa Libya, Abdullah Al-Senussi
Mkuu wa zamani wa upelelezi wa Libya, Abdullah Al-SenussiPicha: AP

Baada ya kuondoka kwa utawala wa Gaddafi, Libya imekuwa ikitawaliwa na serikali ya mpito ambayo ni dhaifu, na machafuko yamekuwa yakiongezeka huku wapiganaji wa zamani wakikaidi amri ya kusalimisha silaha zao. Hali kadhalika wapinzani wenye silaha wamekuwa wakizuia biashara muhimu ya uuzaji wa mafuta nje ya nchi.

Mchakato wa kuimarisha demokrasia katika nchi hiyo umekuwa ukijikokota katika kuweka taasisi za msingi za utawala wa sheria, kwa sababu Gaddafi aliiachia nchi pengo kubwa kiutawala, kwa kuwa alikuwa akiyashikilia madaraka yote mikononi mwake.

Waziri mkuu ajiuzulu

Kesi hiyo inaanza siku moja baada ya waziri mkuu wa mpito, Abdullah al-Thani, kujizulu kufuatia mashambulizi yaliyoilenga familia yake. Alikuwa amekaa madarakani kwa mwezi mmoja tu, akichukuwa nafasi ya mtangulizi wake Ali Zeidan ambaye pia alijiuzulu wadhifa huo.

Mashirika ya haki za binadamu yametilia shaka uwezekano wa hukumu ya haki kwa maafisa wa utawala wa Gaddafi kutoka serikali iliyoingia madarakani baada ya kumuangusha.

Washukiwa katika kesi hii walishitakiwa mahakamani Oktoba mwaka uliopita, na kesi yao ilikuwa imepangwa kusikilizwa Machi 24, lakini iliahirishwa kwa sababu baadhi ya washitakiwa walikuwa hawapo. Miongoni mwa hao ni Seif al-Islam ambaye anashikiliwa kizuizini katika mji wa magharibi wa Zintan.

Uwezekano wa kuahirishwa

Kwa mujibu wa mwendesha mashtaka katika kesi dhidi ya watuhumiwa hawa Seddik l-Sour, kesi hii huenda ikaahirishwa tena, ikisubiri kuwekwa vifaa vya mawasiliano, vitakavyowezesha kuendesha kesi dhidi ya baadhi ya watuhumiwa kwa njia ya video.

Alisema mahakama itafanya uamuzi juu ya kuruhusu matumizi ya kiunganishi cha video kwa watuhumiwa walio katika miji ya Zintan na Misrata. Mwendesha mashitaka huyo alisema pia kuwa kusogezwa mbele kwa tarehe ya kesi hiyo kutawapa baadhi ya watuhumiwa muda zaidi kutafuta mawakili.

Seif al-Islam ambaye aliaminika angekuwa mrithi wa baba yake, alikamatwa na waasi mwezi Novemba mwaka 2011 mjini Zintan na amekuwa akishikiliwa huko. Juhudi za serikali kutaka ahamishiwe katika mji mkuu, Tripoli, zimeambulia patupu.

Yeye na Abdullah Senussi wanatafutwa pia na mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC, kwa tuhuma na uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu. Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limeitolea wito Libya kuwapatia mawakili Seif al-Islam na wenzake kuhakikisha kwamba kesi yao inakuwa ya haki.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/RTRE

Mhariri: Josephat Charo