1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waraka wa uavyaji mimba uliovuja waleta zogo Marekani

Daniel Gakuba
4 Mei 2022

Maandamano yamefanyika Marekani, baada ya kuvujishwa kwa waraka wa maoni, unaoashiria kuwa mahakama ya juu ya nchi hiyo inaweza kufuta sheria ya mwaka 1973 iliyohalalisha uavyaji wa mimba nchini humo.

https://p.dw.com/p/4AoWN
Demonstration für das Abtreibungsrecht in den USA
Baadhi ya waandamanaji wakitetea haki ya kuavya mimba-MarekaniPicha: Morgan Lee/AP/picture alliance

 

Mamia ya waandamanaji waliteremka katika mitaa ya miji kadhaa ikiwemo New York, Atlanta, Chicago, Denver, Los Angeles na Seattle. Walibeba mabango yanayoitaka mahakama ya juu kutoingia katika maamuzi ya wanawake kuhusiana na miili yao.

Chanzo cha yote ni waraka wa maoni ulioandikwa na Jaji Samuel Alito, mmoja wa majaji tisa wa mahakama ya juu ya Marekani, akihimiza kufutwa kwa sheria ya mwaka 1973 iliyoondoa marufuku ya uavyaji wa mimba kote Marekani, maarufu nchini humo kama Roe v. Wade. Jaji Alito alisema anaamini ana maoni sawa na majaji wengine wahafidhina angalau wanne.

Soma zaidi: Maelfu waandamana Marekani kupigania uavyaji mimba

Kwa mara ya kwanza waraka huo wa maoni uliovujishwa ulichapishwa katika jarida la 'Politico' Jumatatu wiki hii, na tayari mahakama ya juu imethibitisha uhalisia wa waraka huo. Jaji mkuu wa Marekani John Roberts amesema uvujishaji wa waraka huo ni mmomonyoko mkubwa wa imani, na ameagiza uchunguzi ili kubainisha ulivyotokea.

Abortion Ban I Oklahoma I Gov. Kevin Stitt
Wale wa mrengo wa kihafidhina wanaamini kuwa kutoa mimba ni kuuwa mtotoPicha: Sue Ogrocki/AP/picture alliance

Mwelekeo wa kihafidhina

Wengi wa majaji katika mahakama ya juu ya Marekani, wakiwemo watatu walioteuliwa na rais wa zamani Donald Trump, ni wahafidhina, wanaoegemea upande unaopinga uavyaji wa mimba, ukisema ni mauaji wa watoto.

Suala la uhuru wa uavyaji wa mimba ni nyeti katika siasa za Marekani, na tayari limeleta mtikisiko katika mpangilio wa maoni kuelekea uchaguzi wa bunge wa katikati mwa muhula wa urais, uchaguzi ambamo wachambuzi wa siasa walikuwa wakitabiri kuwa cha cha Democratic cha Rais Joe Biden kingeshindwa vibaya.

Sasa, Wademocrats wamekuja juu, wakipinga mwelekeo huo wa mahakama ya juu na kuufanya kuwa kauli mbiu ya kampeni yao, wakiwalenga hasa vijana, jamii za wasio wazungu na wanawake wa mijini, makundi ambayo yamekuwa hayapendezwi na yanayojiri chini ya uongozi wa Joe Biden.

Supreme Court Samuel Alito USA Washington
Jaji mhafidhina Samuel Alito, waraka wake wa maoni uliovuja umesababisha mzozoPicha: Erin Schaff/AP/picture alliance

Warepublican washangilia kimya kimya

Warepublican kwa upande wao, wanajaribu kutoonyesha furaha ambayo wangeipata iwapo mahakama ya juu ingefuta sheria ya kuhalalisha uavyaji wa mimba, kitu ambacho wamekuwa wakikipigania kwa zaidi ya muongo mmoja, wakati huo huo wakitumai hautakuwa na gharama kubwa katika uchaguzi ujao.

Soma zaidi: Kavanaugh aapishwa kuwa jaji wa Mahakama ya Juu

Mahakama ya juu inatarajiwa kupitisha uamuzi wake mwishoni mwa muhula wake wa sasa, ama mwishoni mwa mwezi Juni, au mwanzoni mwa Julai.

Rais Joe Biden amewataka wabunge wanaounga mkono uhuru wa wanawake kufanya wapendavyo na miili yao, kuandaa muswada utakaoilinda  uhuru wa wanawake kuamua iwapo wanataka kuavya mimba, kama haki yao kisheria.

 

-ape, rtre