1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kavanaugh aapishwa kuwa jaji wa Mahakama ya Juu

7 Oktoba 2018

 Brett Kavanaugh aliapishwa kuwa jaji wa 114 wa Mahakama ya Juu ya Marekani, baada ya mjadala mkali sana kuhusu tabia chafu ya ngono na majibizano ya kisheria yaliyolitikisa baraza la Seneti na taifa zima.

https://p.dw.com/p/3670p
USA Kavanaugh als Richter am obersten US-Gericht vereidigt
Picha: Reuters//Supreme Court of the United States/F. Schilling

Kuapishwa kwa jaji huyo mwenye umri wa miaka 53 kulikuja katika wakati ambapo Marekani imeingia kwenye kiwango cha juu kabisa cha mpasuko wa kisiasa kati ya waliompinga na waliomuunga mkono, huku ikihofiwa kuwa muhimili wa mahakama utaelemea zaidi kwenye siasa za mrengo mkali wa kulia kwa miongo kadhaa ijayo.

Jaji Kavanaugh aliapishwa kwenye sherehe ya kimyakimya na ya faragha muda mchache baada ya kupata ushindi mdogo kabisa kuwahi kushuhudiwa katika baraza la Seneti kwa takribani karne moja na nusu, huku waandamanaji wakipiga mayowe ya kumpinga nje ya jengo la mahakama.

Ushindi wa kura 50 dhidi ya 48 za kumpinga ulihitimisha mapambano ya muda mrefu ambayo taifa hilo tajiri lilijikuta likipambana nayo ndani yake, baada ya madai kuibuka kwamba aliwahi kuwashambulia kingono wanawake kadhaa miongo mitatu iliyopita - madai ambayo aliyakanusha vikali.

Tuhuma hizi ziliyabadilisha mapambano kutoka yale yanayotafautisha itikadi za kimahakama hado kuwa mashambulizi binafsi juu ya haki za wahanga na wateule na imani ya kutomtia mtu hatiani kabla ya uamuzi wa mahakama.

Trump amkosoa seneta wa Alaska

USA Senat bestätigt umstrittenen Richterkandidaten Kavanaugh | Protest
Maandamano ya kupinga kupitishwa na kuapishwa kwa Brett Kavanaugh kuwa jaji wa Mahakama ya Juu ya Marekani.Picha: Reuters/J. Ernst

Mapema, Rais Donald Trump, ambaye anachukulia huu kuwa ushindi wa wazi kwake, alimshambulia vikali mbunge pekee wa chama chake cha Republican aliyemkataa Kavanaugh, Seneta Lisa Murkowski wa Alaska, akimshutumu kwa kuwa "aibu". 

"Nadhani ilikuwa kura ya kusikitisha sana kabisa. Kwa hakika, nadhani ilikuwa aibu kubwa," Trump aliambia televisheni ya Fox News katika mahojiano kwa njia ya simu.

"Nimeifanyia mengi Alaska, nilishitushwa kumuona akipiga kura ya kupinga. Nadhani itaingia kwenye historia kuwa hii ni siku ya huzuni kwake kwa sababu Kavanaugh atakuja kuwa jaji mzuri kabisa kwa Mahakama ya Juu," aliongeza Trump.

Kwa upande mwengine, Rais Trump alisema anamshukuru Seneta Joe Manchin wa chama cha Democrat, ambaye alikaidi msimamo wa chama chake na kumpigia kura ya kumpitisha Jaji Kavanaugh.

Kabla ya kuzuka kwa madai na shutuma za mashambulizi ya kingono, wajumbe wa Democrat walikuwa wanaupinga uteuzi wa jaji huyo kwa msingi kwamba hukumu na maandiko yake akiwa jaji wa mahakama ya rufaa yalikuwa yanatilia shaka mitazamo yake kuelekea haki za kutoa mimba na haki ya rais kukengeuka uchunguzi wa kisheria.

Kwa vyovyote vile, kuthibitishwa na kuapishwa kwa Jaji Kavanaugh kunachukuliwa kuwa mafanikio makubwa kwa Trump na chama chake cha Republican, ambacho kiliunda nguvu ya pamoja kuhakikisha kuwa kunakuwa na majaji wengi wahafidhina kwenye mahakama hiyo ya juu kabisa. 

Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/dpa
Mhariri: Caro Robi