Makundi ya wapiganaji yadaiwa kuwauwa wengi mwaka huu DRC
6 Agosti 2020Matangazo
Ripoti iliyochapishwa na Ofisi ya Pamoja ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa - UNJHRO inaonyesha kuwa kati ya Januari na Juni 2020, wapiganaji wa makundi yote yenye silaha walihusika na mauaji ya kiholela ya karibu watu 1,315, wakiwemo wanawake 267 na watoto 165.
Hiyo ilikuwa mara tatu zaidi ya 416 ya vifo vya aina hiyo vilivyoorodheshwa katika nusu ya kwanza ya 2019.
Ongezeko hilo ni kutokana na kuzorota kwa hali ya haki za binaadamu katika mikoa ambayo migogoro inatokota, hasa Ituri, Kivu Kusini, Tanganyika na Kivu Kaskazini.
Mashariki ya Congo imekuwa katika machafuko kwa karibu miongo mitatu, ambapo wakaazi wanahangaishwa na makundi ya wapiganaji.