1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanamgambo 18 wauwawa Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo

5 Januari 2022

Jeshi la Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo limetangaza kuwaua wanamgambo 18 wa makundi ya Makanika na Twigwaneho wakati wa mapambano katika vijiji vya Kagogo na Bijombo katika mkoa wa Kivu kusini.

https://p.dw.com/p/45ABJ
Demokratische Republik Kongo Soldaten Patroullie nahe Beni
Picha: picture-alliance/AP Images/Al-Hadji Kudra Maliro

Katika taarifa kwa vyombo vya habari mnamo Jumatano Januari 05, Meja Dieudonné Kaseraka, msemaji wa jeshi katika eneo hilo, alifahamisha kuwa mapigano yalizuka baada ya wanamgambo watiifu kwa afisa wa zamani aliyeasi jeshi, Michel Makanina na Twirwaneho walipojaribu kuvizia kitengo kimoja cha jeshi la FARDC kilichokuwa kinapiga doria katika eneo hilo la wilaya ya Uvira na wakati huo, kitengo hicho cha jeshi la Congo kilifanikiwa kuwaua waasi hao.

Kwasasa hali ya wasiwasi inaendelea kutawala maeneo ya Bijombo na vijiji kadhaa vya Uvira, wakaazi wengi wakiwa wamekimbilia msituni. 

Haya yanajiri wakati huu ambapo duru kadhaa zimeripoti mapigano ya hivi karibuni kati ya jeshi la ulinzi wa kitaifa la Burundi na waasi wa vuguvugu la Burundi la Red Tabara kwenye ardhi ya Congo katika vijiji vya Rurambo kule Gashengo, Nyamarogwe, Rukuka, Kahololo na Bibangwa tangu Jumapili asubuhi katika wilaya hiyohiyo ya Uvira mashariki ya Congo, jeshi la Burundi likiwa limeshirikiana na makundi ya wapiganaji mai-mai ili kulionyesha njia.

soma zaidi:Uganda, DRC wafanya mashambulizi ya pamoja dhidi ya ADF

Mnamo Desemba 23 mwaka jana, wakaazi wa bonde la mto Ruzizi na mashirika ya kiraia ya eneo hilo walithibitisha kwamba wamewaona watu kadhaa wenye silaha wakiwa wamevalia sare za jeshi la Burundi wakielekea nyanda za juu za Uvira.

Hadi sasa jeshi na serikali ya Congo hawajakiri au kukanusha rasmi taarifa hizo. Kwenye mtandao wa kijamii Twitter, Red Tabara wamedai kuwaua askari wa Burundi wakiwataja kuwa "maadui kumi" Jumapili iliopita, mashariki ya Congo.

Mwandishi: Mitima Delachance, DW, Bukavu