Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa waondoka Kaskazini mwa Mali
1 Novemba 2023Waasi wanaotaka kujitenga Kaskazini mwa Mali, wanadai kudhibiti kambi moja iliyokuwa inakaliwa na wanajeshi wa Umoja wa Mataifa katika mji wa kimkakati wa Kidal, hii ikiwa ni moja ya maendeleo makubwa ya waasi hao katika vita vyao vya kudhibiti maeneo ya mji huo.
Haya yanajiri wakati wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja huo MINUSMA wakiondoka mapema katika ngome za waasi Kaskazini mwa taifa hilo, kufuatia kuendelea kuongezeka kwa ukosefu wa usalama na kuuacha mji huo mikononi mwa waasi wa Tuareg.
Myriam Dessables, Mkuu wa kitengo cha mawasiliano wa MINUSMA aliwaambia waandishi habari kwamba, tayari wanajeshi wawili walijeruhiwa katika kambi moja kubwa ya Umoja wa Mataifa mjini Gao, baada ya kushambuliwa kwa mabomu.
Kundi linalofungamana na Al-Qaeda la Jamatu Nusra al-Islam wal-Muslimin, JNIM, lilikiri kuhusika na shambulio hilo.