Wanajeshi wa Ufaransa waitwaa Kidal
30 Januari 2013Kidal sasa unakuwa mji wa mwisho mkubwa kuchukuliwa na wanajeshi wa Ufaransa baada ya kuifikia miji ya Gao na Timbuktu mapema wiki hii, katika kampeni ya kuwang'oa waasi wa Ansar Dine wanaoshukiwa kuwa na mafungamano na al-Qaida.
"Wanajeshi wa Ufaransa waliingia Kidal usiku wa kuamkia leo." Msemaji wa jeshi la Ufaransa, Thierry Burkhard, ameliambia shirika la habari la AFP.
Taarifa hizo zimethibitishwa pia na Rais wa Bunge la Kidal, Haminy Belco Maiga, aliyeliambia shirika la habari la Reuters kwamba wanajeshi hao waliwasili kwenye mji huo wakiwa na ndege nne na helikopta.
Kwa mujibu wa Maiga, hakukuwa na ripoti zozote za wanajeshi hao kukumbana na upinzani kutoka kwa Ansar Dine, lakini akasema kwamba bado operesheni ya kuusafisha mji huo dhidi ya mabaki ya wanamgambo hao ingali inaendelea.
MNLA wataka mazungumzo
Kidal ni mji mkuu wa mkoa wa jangwani wenye jina hilo hilo, ambako inaaminika kuwa wapiganaji hao wa Kiislamu wamekimbilia baada ya mashambulizi ya wiki tatu kutokea angani na ardhini yanayofanywa na jeshi la Ufaransa.
Mapema wiki hii, waasi wa Vuguvugu la Ukombozi wa Azzawad, MNLA, ambao wanapigania uhuru zaidi wa eneo la kaskazini mwa Mali, walitangaza kuuchukua mji huo baada ya Ansar Dine kuondoka.
MNLA mwanzoni iliwahi kushirikiana na Ansar Dine kabla ya kutengana nayo katikati ya mwaka jana, imethibitisha kuwasili kwa wanajeshi wa Ufaransa kwenye mji huo.
Visa vya uvunjaji haki za binaadamu
Wakati hayo yakiendelea, kumekuwa na ripoti za wizi wa ngawira na matukio ya uvunjaji wa haki za binaadamu karibu kwenye maeneo yote yanayokombolewa kutoka mikononi mwa wanamgambo wa Kiislamu sasa.
Mjini Timbuktu, siku moja baada ya wanajeshi wa Kifaransa na Mali kukaribishwa kwa vifijo na nderemo, makundi makubwa ya watu yalivamia na kupora maduka yanayomilikiwa na watu wa jamii za Kiarabu, Mauritania na Algeria, wakidai kwamba waliwaunga mkono Ansar Dine.
Wiki iliyopita, Shirikisho la Kimataifa la Haki za Binaadamu lilizitolea wito serikali za Mali na Ufaransa kuchunguza visa vya mauaji ya makusudi yanayofanywa na wanajeshi wa Mali dhidi ya watu wenye asili za Kiarabu na Kituareg katika maeneo yanayokombolewa na wanajeshi hao.
Shirika hilo limesema lina ripoti za uhakika kuhusu wanaume 12 waliopigwa risasi kwa makusudi na wanajeshi hao, na pia visa vya wanawake kubakwa.
Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AP/AFP
Mhariri: Saumu Yusuf