1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafadhili waipatia Mali zaidi ya dala milioni 455

29 Januari 2013

Maduka yanayomilikiwa na "waarabu" wanaoshirikiana na wafuasi wa itikadi kali yameporwa mjini Timbuktu katika wakati ambapo wafadhili mjini Addis Abeba wameiahidi Mali msaada wa kijeji na kiutu

https://p.dw.com/p/17TaU
Wanajeshi wa Ufaransa na wale wa Mali wanaulinda uwanja wa ndege wa TimbuktuPicha: dapd

Mamia ya watu wamevunja maduka wanayofikiri yanayomilikiwa na watu  kutoka Algeria,na Mauritania wanaotuhumiwa kuwaunga mkono wafuasi wa itikadi kali wanaoshirikiana na mtandao wa kigaidi wa Al Qaida huko Timbuktu.Watu hao wamebeba kila walichokiona,kuanzia televisheni hadi kufikia vyakula na vyombo vya majumbani.Kwa mujibu wa maripota wa shirika la habari la Ufaransa AFP silaha pia zimegunduliwa katika baadhi ya maduka hayo.

Wanajeshi wa Mali hawajakawia kuingilia kati kuzuwia visa vya kupora mali.

Hapo awali shirika linalopigania haki za binaadam Human Rights Watch liliwatolea mwito viongozi wa Mali wachukue hatua zinazohitajika kuwahami wananchi na visa vya kulipiza kisasi.Shirika hilo limezungumzia kitisho cha kuzuka mivutano ya kikabila katika eneo la kaskazini ambako uhasama ni mkubwa kati ya jamii ya watu wenye asili ya kiarabu na ile ya watu weusi  ambao ndio  walio wengi nchini Mali.

Wafadhili waahidi msaada wav kijeshi na kiutu

Mali Geberkonferenz in Addis Abeba 29.01.2013
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa Laurent Fabius akihutubia mkutano wa wafadhili mjini Addis AbebaPicha: Simon Maina/AFP/Getty Images

Wakati huo huo mjini Addis Abeba nchini Ethiopia,wawakilishi wa Umoja wa Afrika,Umoja wa ulaya,Japan,Marekani na Umoja wa Mataifa wakihudhuria mkutano wa wafadhili ,wamekubali kuipatia Mali msaada wenye thamani ya dala milioni 455.53 kukidhi mahitaji ya kijeshi na kiutu.

"Hali inahitaji jibu  thabiti na la haraka la kimataifa,kwasababu inatishia usalama wa Mali,eneo,bara na hata zaidi ya hapo" amesema mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Afrika,bibi Nkosazana Dlamini Zuma.

Matamshi kama hayo yametolewa pia na rais Boni Yayi wa Benin aliposema:"Ni suala linalolihusu eneo lote la Sahel na Sahara.Kwasababu ni suala la kupatikana amani na utulivu.Tunataka kusisitiza,tunahitaji amani na utulivu ili kuwa na mustakbal mwema.

Wakati huo huo wanajeshi 3500 wa Ufaransa na 1900 wa kiafrika wakiwemo wa Tchad na Niger wanaakutikana nchini Mali wakisaidiana na wanajeshi wa nchi hiyo.

Rais wa mpito aahidi uchaguzi haraka

Dioncounda Traore
Rais wa mpito wa Mali Dioncounda TraorePicha: AFP/Getty Images

Mjini Timbuktu,kuna uhaba wa chakula na ukosefu wa,umeme,maji na mawasiliano ya simu yaliyokatwa na waasi kabla ya kukimbia .

Rais wa mpito wa Mali Dioncounda Traoré amesema mjini Addis Ababa anataraji kuitisha uchaguzi haraka iwezekanavyo nchini mwake.Hilo ni mojawapo ya masharti yaliyotolewa na wafadhili katika mkutano wao mjini humo  hii leo.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman