Wanajeshi 15 wauwa na Boko Haram
10 Machi 2015Kwa mujibu wa duru moja ya kijeshi, operesheni hii inatajwa kuwa mafanikio ya kwanza katika operesheni ya mashambulizi ya pamoja iliyotokelezwa na wanajeshi kutoka mataifa hayo mawili. Duru zinaeleza kuwa kiasi ya wanajeshi wengine 30 kutoka Chad na Nigeria wamejeruhiwa katika mapigano katika mji wa Malam na Fatouri na Damasak.
Sababu za operesheni
Tukio hilo limekuja siku moja baada ya maelfu ya wanajeshi kuvuka na kuyadhibiti maeneo ambayo yamekuwa yakishikiliwa na wapiganaji wa Kiislamu, wenye itikadi kali ambao vurugu zao zimelisababishia taifa la Nigeria kuchelewesha uchaguzi na mataifa jirani kuunganisha nguvu ya pamoja ya kijeshi katika kukabiliana na kundi hilo.
Afisa mmoja wa Chad ambae hakutaka kutajwa jina, alisema kiasi yawanajeshi 10 wa Chad wameuwawa na wengine 20 wamejeruhiwa katika purukushani za kuikomboa miji hiyo. Vyanzo vingine viwili tofauti kwa upande wa jeshi la Nigeria vililiambia shirika la habari la Ufaransa wanajeshi watano wameuwawa katika mapigano hayo.
Hata hivyo mpaka sasa hakujawa na taarifa rasmi kutoka kwa pande zote mbili zinazoshiriki operesheni hizo.
Nukuu kutoka jeshini
Afisa wa jeshi wa Niger amenukuliwa alisema "Tumewaondosha kabisa maadui zetu katika maeneo haya na kwa hivi sasa yapo katika udhibiti wetu"
Askari hiyo aliendelea kusema vikosi vilivyokuwa katika mstari wa mbele katika uwanja wa mapambano vimefanikiwa kukamata shehena kubwa ya silaha na hivi sasa vinaendelea na zoezi la kusafishasafisha maeneo hayo ili yaendelea kuwa salama kabisa. Vilevile mtoa taarifa huyo alisema wamefanikiwa kuwaweka kuwakamata wapiganaji kadhaa wa kundi la Boko Haram.
Damasak, ni mji wa Nigeria uliopo mji ulio umbali wa kilometa 10 kusini mwa mpaka wa taifa hilo na Niger, ambako wanajeshi wa Chad na Nigeri waliweka kambi kwa wiki kadhaa, kabla ya kufanya mashambulizi hayo makubwa.
Wanajeshi 30 hospitalini
Vyanzo kutoka katika hosiptali iitwayo Diffa, iliyopo katika mkoa wa Niger Delta, ambao unapakana na eneo lijulikanalo kama ngome ya Boko Haram, huko kaskazini mwa Nigeria vimeeleza askari hao 30 waliojeruhiwa wamelazwa katika hospitali hiyo.
Chanzo kingine cha habari kutoka jeshini kinadaia kiasi ya wapiganaji 300 wa Boko Haram wameuwawa. Duru za habari hiyo zilizotolewa na shirika la habari la Uingereza Ruters, zinasema mpaka sasa hakujawa na uthibitisho rasmi wa vifo hivyo na haijawa rahisi kuweza kuhakiki takwimu za mauwaji hayo.
Mataifa ya Cameroon, Chad, Niger na Benin yamejumuisha nguvu ya pamoja ya kujeshi kwa lengo la kuisadia Nigeria kukabiliana na Boko Haram baada ya kuteka sehemu kubwa ya maeneo ya taifa hilo na kufanya mashambulizi katika maeneo ya mipaka na nchi hizo jirani
Mwandishi: Sudi Mnette RTR
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman