1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanaharakati waonya unyanyasaji wa wanawake, Pakistan.

Saleh Mwanamilongo
30 Julai 2021

Mashirika ya haki za binadamu nchini Pakistan yameonya kuhusu ongezeko la mashambulizi na visa vya unyanyasaji dhidi ya wanawake.

https://p.dw.com/p/3yKmG
Pakistan Islamabad | Internationaler Frauentag 2019
Picha: Aamir Qureshi/AFP/Getty Images

Mashirika ya haki za binadamu nchini Pakistan yameonya kuhusu ongezeko la mashambulizi na visa vya unyanyasaji dhidi ya wanawake. Pakistan ni moja ya nchi zinazoshika mkia katika usawa wa jinsia ulimwenguni kwa mujibu wa orodha ya jukwaa la uchumi la dunia, WEF.

Saa za mwisho za maisha ya Noor Mukadam zilikuwa za kuogofya sana. Baada ya kupigwa mfululizo, msichana huyo aliekuwa na umri wa miaka 27 alijaribu kutoroka kwa kuruka kupitia dirisha lakini alirejeshwa na kupigwa tena na hatimaye kukatwa kichwa. Rafiki yake wa utotoni amefunguliwa mashtaka ya kuhusika na mauwaji yake.

Kifo hicho cha kutisha kilichotokea wiki iliopita kwenye maeneo ya starehe nje ya jiji la Islamabad ni tukio la hivi karibuni katika mfululizo wa mashambulizi dhidi ya wanawake nchini Pakistan. Nchi ambayo wanaharakati wa haki za binadamu wamesema visa kama hivyo vya dhuluma dhidi ya wanawake vinaongezeka, huku nchi hiyo ikushuhudia kusambaa kwa itikadi kali za kidini.

Mukadam alikuwa binti ya mwanadiplomasia, na hadhi yake kama mwanachama wa tabaka la wasomi nchini humo imetoa fursa ya kumulikwa kwa ongezeko la ukatili dhidi yawanawake nchini Pakistan alisema Tahira Abdullah, mwanaharakati mashuhuri wa haki za binadamu nchini humo.

Pakistan I Protest gegen Gewalt an Frauen
Wanawake wakiandamana kupinga vitendo vya ubakaji nchini Pakistan.Picha: Arif Ali/AFP/Getty Images

Lakini idadi kubwa ya wanawake wahanga wa dhuluma hizo ni kutoka jamii za matabaka masikini au ya za pato la kati na mara nyingi vifo vyao haviripotiwi, au vinaporipotiwa, hupuuzwa.

Abdullah amesema anaorodha ndefu ya wahanga wa visa hivyo mnamo kipindi cha wiki moja pekee. Amesema janga la uhalifu dhidi ya wanawake nchini Pakistan ni janga lisilo zungumziwa. Hakuna analoliona na hakuna anaelizungumzia, aliendelea kusema Abdullah.

Bunge la Pakistan lilishindwa kupitisha muswada wa sheria inayowalinda wanawake dhidi ya dhuluma za nyumbani, vikiwemo vipigo kutoka kwa waume zao. Badala yake,bunge lililiomba baraza la kidini kushughulikia hatua hiyo, baraza hilo hilo ambalo awali lilielezea kuwa sio kosa mwanaume kumpiga mke wake.

Ripoti ya shirika la Human Rights Watch inasema data zilizo kusanywa na idara ya kuorodhesha visa vya dhuluma dhidi yawanawake nchini Pakistan zinaonyesha ongezeko la asilimia mia mbili ya dhuluma za nyumbani baina ya mwezi Januari na mwezi Machi mwaka jana.

Idadi ya dhuluma hizo iliongezeka zaidi wakati wa vizuwizi vya kupambana na janga laCovid-19 inaelezea ripoti hiyo.

Pakistan Islamabad | Imran Khan, Premierminister
Waziri mkuu wa Pakistan Imran Khan analaumiwa kwa kushindwa kukemea unyanyasaji dhidi ya wanawake.Picha: Saiyna Bashir/REUTERS

Mwaka 2020, Pakistan ilikuwa miongoni mwa mataifa manne yaliyoshika nafasi ya mwisho ulimwenguni katika usawa wa jinsia. Kwa mujibu wa faharasi ya jinsia ya Jukwaa la kiuchumi la duniani WEF, Pakistan inashika nafasi ya 153 miongoni mwa nchi 156 katika usawa wa jinsia, ikifuatiwa na Irak, Yemen na Afghanistan ilioshika nafasi ya mwisho. Hali hiyo ni licha ya mabilioni za dola kuwekezwa na jumuiya ya kimataifa kuhusu usawa wa jinsia miaka 20 iliopita kwenye nchi hizo.

Visa vingi vya unyanyasaji dhidi ya wanawake nchini Pakistan vinadhaniwa kuwa ni mauwaji yanayofanywa na ndugu wa kiume wa familia kwa madai kwamba wahanga hao wamedhalilisha familia. Wanaharakati wa haki zabinadamu wamesema kila mwaka zaidi ya wanawake 1000 wanauliwa kwa njia hiyo, na visa hivyo haviripotiwi.

Mashirika ya haki za binadamu yamekuwa yakimkosoa Waziri Mkuu wa Pakistan, Imran Khan na serikali yake yakisema anaegemea zaidi haki za kidini na kuyafumbia macho makosa ya uhalifu dhidi ya wanawake.

Septemba mwaka uliopita, afisa moja wa polisi alimlaumu mwanamke alievamiwa na kubakwa mbele ya wanaye wawili akisema asinge safiri usiku bila kusindikizwa na mwanaume.

Amir Rana wa taasisi ya amani nchini Pakistan anasema kauli kama hiyo inabainisha ongezeko la misimamo mikali ya kidini nchini Pakistan.

Sikiliza Zaidi: 

Visa vya mauaji na ukatili wa kijinsia kwa wanawake Tanzania

Mwandishi: Saleh Mwanamilongo