1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waliokufa katika mafuriko Afrika Kusini wafikia 259

Sylvia Mwehozi
14 Aprili 2022

Idadi ya watu waliopoteza maisha katika mafuriko kwenye maeneo ya mji wa Durban nchini Afrika Kusini imepanda na kufikia 259 huku mamlaka nchini humo zikionya kwamba watu wengi zaidi bado wanahofiwa kupotea.

https://p.dw.com/p/49uxE
BG Südafrika | Erdrutsch Überflutung
Picha: ROGAN WARD/REUTERS

Mvua zilizonyesha kwa siku kadhaa zimesababisha maporomoko ya udongo na kusomba makaazi ya watu. Idadi ya waliofariki inatarajiwa kuongezeka wakati zoezi la utafutaji na uokoaji likiendelea katika jimbo la KwaZulu-Natal. Raia wengi wa maeneo hayo wamelazimika kuyakimbia makaazi yao ambayo yamesombwa na maji, majengo kuporomoka na miundombinu ya barabara kuharibika vibaya. Bandari ya Durban ilifurika maji na kontena za meli kusombwa.

Überschwemmung in Südafrika
Moja ya daraja lililoharibiwaPicha: AP/picture alliance

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amesema mafuriko hayo ni "janga kubwa sana", akiongeza kuwa "maafa haya ni sehemu ya mabadiliko ya tabia nchi". Ramaphosa ametembelea maeneo yaliyoathirika vibaya na mafuriko ya Durban na maeneo jirani ya jiji kuu la eThekwini. Mkoa wa KwaZulu Natal unatarajiwa kutangazwa eneo la maafa.

Mamlaka pia zinajaribu kurejesha umeme katika maeneo mengi ya jimbo hilo baada ya mafuriko makubwa katika vituo mbalimbali vya kuzalisha umeme. Juhudi za uokoaji za jeshi la ulinzi la kitaifa la Afrika Kusini zilitatizika kutokana na kitengo chake cha jeshi la anga pia kuathiriwa na mafuriko. Mamlaka ya hali ya hewa ya Afrika Kusini imeonya kuendelea kwa hali ya upepo na mvua na hatari ya mafuriko huko Kwazulu-Natal na mikoa mingine wakati wa sikukuu ya Pasaka. Mikoa ya Eastern Cape, Free State na majimbo ya Kaskazini Magharibi inaweza kuathirika.