1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakimbizi wa Syria wafikia milioni 2

Admin.WagnerD3 Septemba 2013

Umoja wa Mataifa umesema kwamba vita nchini Syria vimeshawalazimisha raia milioni 2 kuikimbia nchi hiyo na kuwageuza wengine milioni 4 kuwa wakimbizi wa ndani huku Marekani ikiwa inajiandaa kuivamia Syria.

https://p.dw.com/p/19abi
UN High Commissioner for Refugees (UNHCR) Antonio Guterres speaks during a press conference in Amman, on the Syrian refugee crisis, on March 13, 2013. More than a million Syrians have registered abroad with the UNHCR. AFP PHOTO/STR (Photo credit should read -/AFP/Getty Images)
Antonio Guterres UNHCR 13.03.2013 in AmmanPicha: AFP/Getty Images

Kwa mujibu wa Mkuu wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, "Syria imegeuka kuwa msiba mkuu kabisa wa zama hizi na janga la kibinaadamu linalotia aibu." Guterres ameyasifu mataifa jirani kwa kukubali kuwapokea na kuwapa hifadhi wakimbizi hao, na hivyo kuokoa roho za maelfu ya watu.

Mashahidi wameripoti misafara mikubwa zaidi ya Wasyria wanaomiminika kwenye nchi jirani, tangu onyo la Rais Barack Obama wa Marekani la wiki iliyopita, kwamba yuko tayari kuushambulia utawala wa Bashar al-Assad kijeshi, kutokana na tuhuma za matumizi ya silaha za kemikali.

Obama anatafuta uungwaji mkono wa bunge la nchi yake kwa hatua ya kijeshi dhidi ya Syria, huku akiahirisha kwa muda uvamizi huo kuwapa muda raia kuihama nchi hiyo.

Wakimbizi 5,000 kwa siku

Takribani raia 5,000 huikimbia Syria kila siku, wengi wao wakiwa hawana chochote zaidi ya nguo walizovaa, na Guterres amesema kinachotia hofu zaidi, ni kwamba idadi ya wakimbizi imechupa kufikia milioni 1.8 kwa kipindi cha miezi 12 tu, kutoka ile ya 231,000 mwaka jana.

Rais Barack Obama na Makamu wake Joe Biden.
Rais Barack Obama na Makamu wake Joe Biden.Picha: Reuters

Hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Agosti, Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa lilihisabu wakimbizi 716,000 wa Syria nchini Lebanon, 515,000 nchini Jordan, 460,000 Uturuki, 168 Iraq na 110,000 nchini Misri. Kwa mujibu wa shirika hilo, zaidi ya nusu ya wakimbizi hao ni watoto wadogo.

Idadi hii ni sawa na asilimia 97 ya wakimbizi wa Syria, na hali hiyo imeifanya miundombinu, uchumi na jamii kwenye mataifa jirani kuzidiwa nguvu na hivyo kuhitaji msaada wa haraka kutoka jumuiya ya kimataifa. Mawaziri kutoka nchi hizo wanatarajiwa kukutana na Guterres leo mjini Geneva, Uswisi, katika jitihada za kutafuta msaada mkubwa zaidi wa kimataifa.

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa wakimbizi, muigizaji wa filamu Angelina Jolie, amesema kwamba ikiwa hali itaendelea kuzorota kwa kiwango cha sasa, basi "idadi ya wakimbizi itaongezeka na baadhi ya nchi jirani zitafikia kiwango cha kuporomoka."

Marekani ruhusa ya kuivamia Syria

Katika hatua nyengine mawaziri wa mambo ya nje na ulinzi wa Marekani watakutana na jopo la baraza la Seneti hivi leo kutoa ushahidi mbele ya Kamati ya Mambo ya Nje ya Seneti wa kuthibitisha uhalali wa Marekani kuivamia Syria kijeshi.

Wakimbizi wa Syria.
Wakimbizi wa Syria.Picha: Bulent Kilic/AFP/Getty Images

Seneta John McCain kutokea chama cha Republican anaunga mkono uvamizi huo.

"Kukataa jambo hilo nadhani kutakuwa na madhara makubwa kwa sababu kutahujumu heshima ya Marekani, na si rais wa Marekani sisi wenyewe tunaotaka hilo litokee."

Kwa upande wake, Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amesema hivi leo kwamba anatarajia makubaliano ya kimataifa juu ya Syria yatafikiwa kwenye mkutano wa wiki hii kundi la mataifa 20, G20.

Merkel, ambaye amerejelea mara kwa mara kwamba nchi yake haitashiriki kwenye mashambulizi yatakayoongozwa na Marekani dhidi ya utawala wa Assad, ametoa wito wa kufanyika kwa jitihada mpya za kuishawishi mwenyeji wa mkutano huo, Urusi, kuunga mkono matokeo yoyote dhidi ya Syria.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AP/AFP
Mhariri: Saumu Yusuf