Ufaransa kujadili uingiliaji kati Syria
3 Septemba 2013Uingereza imejitoa baada ya wabunge kupinga hatua dhidi ya Syria. Marekani nayo, inataka pia kupata idhini kutoka kwa wabunge wake , hali ambayo matokeo yake hayajulikani. Ufaransa kwa muda wa siku kadha sasa inajaribu kuweka muungano wa kuishambulia serikali ya Bashar al-Assad, na majadiliano yamekuwa makali.
Bunge la Ufaransa linataka kujadili suala hilo na kutoa maamuzi kupitia vyama vyote. Kwa Ufaransa hata hivyo kuna wingi wa kutosha kufikia makubaliano, lakini wabunge wanajiuliza ni vipi itawezekana?
Mawazo yatofautiana
Si kawaida kwamba mawazo ya wengi yanakwenda kinyume na nia ya rais, amesema mwenyekiti wa chama cha upinzani cha UMP Jean-Francois Cope. Rais Hollande anawajibika kutoa ufafanuzi wa hali ilivyo kwa sasa pamoja na mipango yake.
Alain Juppe kiongozi mmojawapo mwenye ushawishi kutoka upinzani , ambaye aliwahi kuwa waziri wa mambo ya kigeni anapendelea kuingilia kijeshi nchini Syria. Pamoja na hayo anataka kwanza bunge lijadili na kutoa maamuzi. Itakuwa mara ya kwanza kwa Ufaransa kuingilia kati bila ya kupata idhini ya Umoja wa Mataifa.
Hii itakuwa ukiukaji wa sera zetu hadi sasa. Lakini nafikiri itatosha kwa bunge kuidhinisha, amesema Juppe.
Katiba haimlazimishi rais wa Ufaransa kupata idhini ya bunge kwenda vitani, anasema mbunge wa chama cha Kisoshalist Matthias Fekl alipozungumza na DW. Ama katiba pia haimlazimishi kuitisha kikao cha bunge kwa ajili ya suala kama hilo.
Hollande kufafanua hali ilivyo
Lakini rais Francois Hollande ameitisha kikao maalum cha bunge kesho Jumatano(04.09.2013). Anataka kulifahamisha bunge juu ya hali ilivyo nchini Syria pamoja na msimamo kwa upande wa kidiplomasia.
Haki ina upande mmoja tu. Pamoja na hayo kuna hali ya dharura, kuweza kujenga muungano na kupeleka majeshi kupambana nchi za nje, na kwamba sio uamuzi uliochukuliwa na nchi pekee, amesema mbunge wa bunge la Ujerumani anayezifahamu siasa za Ufaransa Andreas Schockenhoff. Nafahamu ulazima wa bunge la Ufaransa kukutana na kujadili suala hili, ameongeza mbunge huyo.
Inaonesha kuwa katika masuala kama haya wananchi pamoja na wabunge wao si lazima kuwa wana mawazo yanayofanana, ameeleza Schockenhoff katika mahojiano na DW. Hata katika mataifa ambayo katiba haijaeleza wazi juu ya mjadala wa bunge , kuna hali ya kupendelea mjadala wa wazi.
Mbunge wa Ufaransa Matthias Fekl ameongeza kuwa hakuna mtu anayetaka vita lakini kutokana na hili lililotokea Ufaransa inawajibu wa kuchukua.
"Wafaransa wana hisia sawa kama Wajerumani. Hatutaki vita, hatutaki uingiliaji kati kijeshi kwa gharama yoyote ile. Lakini hatutaki pia kuona wauaji wakiachwa bila kuadhibiwa".
Majeshi tiifu kwa rais Bashar al-Assad yamefanya shambulio la silaha za kemikali mwezi uliopita, ripoti ya kijasusi ya Ufaransa imesema, huku kiongozi huyo wa Syria akionya kuwa shambulio la kijeshi dhidi yake huenda likazusha vita vya eneo hilo lote.
Mwandishi : Heinze , Hendrik / ZR / Sekione Kitojo
Mhariri: Hamidou Oummilkheir