Wakaguzi wa UN wawasili Syria kuchunguza silaha za sumu
24 Julai 2013Taarifa kutoka Umoja wa Mataifa zinasema wakaguzi hao walipangiwa kukutana na maafisa wa serikali ya Syria kujadili namna ya kuingia katika maeneo ambako silaha hizo zilidaiwa kutumiwa.
Ziara hii inakuja baada ya Umoja wa Mataifa kukubali mualiko kutoka serikali ya rais Bashar al-Assad mweji Juni, kufanya uchunguzi katika mji wa Khan al Assal, uliyopo katika mkoa wa kaskazini wa Alleppo, ambako silaha za kemikali ziliripotiwa kutumiwa. Mji wa Khan al-Assal ndiyo ulikuwa eneo la mapigano makali mwezi Machi kati ya vikosi vya serikali na waasi. Pande zote mbili zilishtumiana kwa kufanya shambulizi baya la kemikali dhidi ya mji huo.
Mkutano kati ya Jarba na Hollande
Upinzani umeurejesha mji wa Khan al-Assal mapema wiki hii. Uingereza, Ufaransa na Marekani zimetoa ushahidi katika miezi ya hivi karibuni, juu ya mashambulizi mengine yanayoshukiwa kuwa ya kemikali nchini Syria, ambayo wanavishtumu vikosi vya rais Assad kwa kuyafanya. Mjini Paris, kiongozi wa muungano wa upinzani wa baraza la taifa la Syria SNC Ahmad al-Jarba, alitarajiwa kuwa na mazungumzo na rais Ufaransa Francois Hollande baadae leo, kuhusu suala nyeti la kuwapatia waasi silaha.
Ufaransa ilikuwa nchi ya kwanza kuutambua muungano huo mwaka jana, na hivi karibuni, kuthibitsha matumizi ya silaha za sumu na utawala wa Assad. Hata hivyo, serikali ya Ufaransa imekuwa ikisita juu ya suala la kuwapatia silaha waasi, kwa sababu haijapata uthibitisha tosha kuwa silaha hizo hazitaishia mikononi mwa makundi yenye itikadi kali yanayopambana dhidi ya utawala wa Assad.
Al-Jaraba aliwasili mjini Paris siku ya Jumanne, katika mwanzo wa ziara yake itakayomfikisha pia mjini New York nchini Marekani baadae wiki hii kwa ajili ya mazungumzo na wanachama wa baraza la uslama la Umoja wa mataifa, ikiwemo Urusi.
Bunge Marekani launga kuingilia kijeshi Syria
Baada ya utawala mjini Washington kuthibitisha wiki kadhaa zilizopita kuwa msitari mwekundu ulikuwa umevukwa kwa kutumia silaha za kemikali, serikali ya Marekani ilianza kufanya mipango ya kutoa msaada wa kijeshi kwa makundi ya waasi. Siku ya Jumanne maafisa wa bunge la Marekani waliashiria kuunga mkono wa mpango ulioainishwa katika barua kutoka kwa Jenerali wa juu kabisa wa Pentagon Martin Dempsey, mwenyekiti wa vikosi vya ulinzi na usalama vya Marekani.
Katika barua hiyo, Dempsey alibainisha njia na hatari zilizopo kwa Marekani kutoa msaada wa kijeshi kwa waasi, na kusema zinaweza kuwa na ufanisi, lakini pia zina gharama kubwa - kwani zitahitajika dola bilioni moja kila mwezi kuweka eneo lisiloruhusiwa ndege kuruka, na kuonya juu ya madhara yasiyokusudiwa kwa hatua watakazozichukua, iwapo utawala wa Assad utaanguka bila kuwepo na upinzani imara. Mabaraza yote ya bunge yaliidhinisha mpango wa Dempsey.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/dpae,
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman