Kiongozi wa waasi Syria akutana na rais Hollande
24 Julai 2013Kiongozi huyo mpya wa upinzani Ahmad Jarba, aliwaambia waandishi wa habari baada ya kukutana na wajumbe wa kamati ya mambo ya nje ya bunge la Ufaransa jana Jumanne, kuwa suala la kuomba msaada wa kijeshi ni moja ya malengo ya ziara yake ya siku mbili nchini Ufaransa.
Mkuu wa Jeshi Huru la Syria Jenerali Selim Idriss, aliongeza kuwa upinzani ulikuwa unafanyakazi na washirika wao wa Ulaya na Marekani ili kupata msaada wa kiufundi, afya na kibinaadamu, na kuongeza kuwa wanatumaini pia watapatiwa msaada wa silaha kwa kuwa waasi hawana zana za kutosha.
Hii ndiyo ziara ya kwanza ya Jarba nchini Ufaransa tangu alipochaguliwa kuwa kiongozi wa muungano wa upinzani wa Syria SNC Julai 6, na alisema mwaliko wa rais Hollande ni ushahidi kuwa Ufaransa ina maslahi katika hatma ya Syria. Baada ya Ufaransa, Jarba ataelekea mjini New York Marekani kwa ajili ya mikutano katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa. Uingereza ilisema baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lenye wanachama 15 zikiwemo Urusi na China, litafanya mkutano wake wa kwanza na uongozi wa SNC siku ya Ijumaa.
Maafisa wa Ufaransa walisema mazungumzo na wapinzani yalikuwa yanapangwa kufanyika katika miji ya London na Berlin. Afisa wa juu wa Umoja wa mataifa alisema kuwa umoja huo umearifiwa kuhusu mashambulizi 13 yanayohusisha silaha za kemikali nchini Syria. Wataalamu wawili wa umoja huo walitarajiwa kuwasili mjini Damascus hii leo, kwa ajili ya mazungumzo na serikali.
Waasi wauteka mji muhimu wa Khan al-Assal
Lakini matumaini ya Umoja wa Mataifa kuchunguza matumizi ya silaha hizo yalipata pigo, baada ya waasi kuuteka mji muhimu wa Khan al-Assal kutoka kwa vikosi vya Assad siku mbili kabla ya kuwasili mjini Damascus kwa Ake Sellstrom, mkuu wa jopo la wachunguzi, na Angela Kane, ambae ni mkuu wa kitengo cha kupunguza nguvu za silaha cha Umoja wa Mataifa.
Mji wa Khan al-Assal ndiyo ulikuwa eneo la shambulizi baya la Machi 9, ambalo serikali ilisema lilifanywa na waasi ilipoutaka umoja wa mataifa kufanya uchunguzi. Mwanadiplomasia wa Umoja wa Mataifa, alisema itakuwa vigumu kwa wataalamu hao kuruhusiwa kuingia katika mji kama hauko katika udhibiti wa serikali.
Mataifa yote makubwa yanakubali kuwa silaha za kemikali zimetumiwa nchini Syria katika mgogoro uliyodumu miezi 28 sasa. Lakini mzozo kuhusu upande gani umetumia silaha hizo umekuwa chanzo kipya cha mgawiko juu ya Syria.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe
Mhariri: Saum Yusuf