1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wajumbe wa mazingira wajadiliana juu ya makubaliano ya Basel

23 Juni 2008

Takataka za sumu zahatarisha maisha ya watu kwenye nchi maskini

https://p.dw.com/p/EPW3

Takataka hatari za sumu mara nyingi hutokea katika nchi za magharibi za viwanda na takataka hizo huishia kutupwa kwenye nchi za nje zinazoendelea. Hatua hiyo ni kinyume na sheria na pia ni hatari kwa maisha ya binadamu. Katika mkutano unaofanyika wiki hii huko Bali Indonesia viongozi wa nchi zilizotia saini makubaliano ya Basel watajadiliana juu ya jinsi ya kulitatua tatizo hili. Takataka zinazotoka majumbani kwenye nchi za magharibi za viwanda hutakiwa kutupwa ,kusafirishwa kwenye depo au kuchomwa moto na hata kubadilishwa katika hali nyingine ya kuweza kutumika. Na jambo hili halipasi kuwa vinginevyo. Hata hivyo hali sio namna hiyo kwani takataka hizo nyingi huishia kutupwa katika nchi za nje zinazoendelea na hii sio tu ni kinyume cha sheria lakini pia ni uchafuzi wa mazingira na hatari kwa maisha ya binadamu. Masuala kama hayo ni miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa katika kikao cha tarehe 23 hadi 25 cha maadhimisho ya kutiwa saini kwa mkataba wa Basel makubaliano ambayo yanatia shime kurekebishwa kwa hali ya mambo kuhusiana na uchafu huo wa sumu. Tangu mwaka 1994 mashirika ya mazingira yamekuwa yakiyataka mashirika yanayohusika na takataka hizo kurekebisha hali ya mambo na wakati huohuo kutafuta makubaliano mapya ya utaratibu wa sera zitakazosaidia usafirishaji na utupaji wa takataka ambazo ni hatari.

Mara nyingi takataka hatari zinaishia kwenye nchi kama vile India na Bangladesh ambako hali inadhihirika wazi unapoingia kwenye fukwe za bahari za nchi hizo unakumbana na mabaki ya meli zilizoharibika,barani Afrika hali pia ni hiyo hiyo ambapo mitambo ya computa mbovu na simu za mikononi zilizoharibika zinaishia kwenye eneo hilo.Na daima utakumbana na wafanyikazi ambao wanashughulikia kuvirekebisha vifaa hivyo vibovu huku wakiwa wamevalia vifaa malum vya kujikinga na sumu ilmradi mtaji unaingia.

Itakumbukwa kwamba mwaka 2006 uholanzi ilijikuta imeingia katika kashfa kubwa wakati meli yake iliyobeba takataka za sumu kiasi tani 500 ilipozimwaga kwenye pwani ya Cote divore barani Afrika jambo ambalo lilikosolewa sana kimataifa.Kashfa kama hizo hata hivyo kwa sasa zimepungua tangu kufikiwa makubaliano ya mwaka 1980 makubaliano ambayo yalianza kufanya kazi mwaka 1994. Makubaliano hayo yametilia mkazo kufuatwa sheria katika utupaji wa takataka hatari kwa mfano takataka zinatokana na madawa ya mahospitali,betteri,mafuta machafu na takataka za kemilkali. Joachim Wuutke mjumbe maalum wa ujerumani anayehusika na makubalianao ya Basel na anayefanya kazi katika wizara ya shirikisho ya mazingira amesema ''kuna tatizo kubwa ambalo linahusiana na utupaji wa takataka za sumu zingatio ni kwamba ni ufafanuzi iwapo ni taka au ni zana za bidhaa ambazo sio rahisi kuzidhibiti.''

Bwana Wuttke ameongeza kusema kwamba kuna tofauti kubwa kuhusiana na suala la iwapo tushirikiane kwa kufanya kazi chini ya utaratibu mmoja wa kuyaweka masuala yote ya mkataba huo wa Basel katika mfumo mmoja.

Ni kutokana na hali kama hiyo mkutano huo utakaofanyika mjini Bali Indonesia ambapo wawakilishi kutoka nchi 170 watahudhuria watajadiliana pia juu ya kupatikana ushirikiano huru na wa sawa kati ya pande zote husika za mazingira.

Wajumbe watazungumzia masuala ya kisheria kuhusiana na marufuku ya kusafirisha takataka chini ya mkataba wa Basel.

Mara kwa mara watoto wamekuwa waathirika wakubwa wa madhara yanayotokana na takataka hizo za sumu zinazotupwa kinyume cha sheria hivyo inabidi paweko mikakati ya kuzuia hatari hiyo kama anayosisitiza Klaus Koch kutoka mtandao wa wanamazingira nchini Ujerumani amefafanua kwamba ''Wakati Watoto wanapokulia kwenye hali kama hii wanapata madhara na hivyo kusababisha maisha mafupi na wakibahatika kuwa watu wazima kama wanafikia huko wanahatari kubwa ya kuugua saratani.''

Mkutano huo wa bali unatarajiwa kutoa azimio la Bali linalolenga kuweka umuhimu juu ya suala la afya na usimamizi wa utupaji taka kwa ajili ya kufikia mikakati ya maendeleo ya dunia kama vile kuupunguza umaskini.

►◄