Wajumbe wa COP27 wakubaliana kuzisaidia nchi maskini
20 Novemba 2022Makubaliano ya kuundwa kwa mfuko wa kuzifidia nchi maskini zinazoathiriwa na uchafuzi wa gesi ya kaboni unaosababishwa na nchi tajiri, yamefikiwa Jumapili asubuhi katika kikao cha mashauriano kwenye mkutano huo unaofanyika kwenye mji wa mapumziko wa Sharm el-Sheikh nchini Misri.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Sameh Shoukry ambaye pia ni Rais wa COP27, alipendekeza kuanzishwa kwa mfuko huo Jumamosi mchana na kufikiwa na pande husika siku hiyo hiyo. Shoukry aliyatangaza makubaliano hayo mapema Jumapili.
Hata hivyo makubaliano makubwa bado hayajafikiwa kwa sababu ya mvutano uliopo kuhusu juhudi za kupunguza matumizi ya gesi ya kaboni inayochafua mazingira.
Maamuzi muhimu juu ya kuachana na nishati zote za mafuta na makaa ya mawe na kuweka kikomo cha ongezeko la joto kwa nyuzi joto 1.5 katika kipimo cha Celsius, kilichokubaliwa katika katika mkutano wa COP26 uliofanyika mwaka uliopita huko Glasgow, bado hayajafikiwa.
Mfuko huo uliopewa jina "hasara na uharibifu" umekuwa ajenda rasmi kwa mara ya kwanza katika mkutano wa kilele wa COP27, baada ya shinikizo kuongezeka kutoka katika nchi zinazoendelea.
Wajumbe wamepongeza kuanzishwa kwa mfuko huo kufuatia wiki mbili za mazungumzo yenye utata kuhusu matakwa ya mataifa yanayoendelea kwa mataifa tajiri ambayo ni wachafuzi wa mazingira, kuwafidia kutokana na uharibu na majanga yanayosababishwa na hali mbaya ya hewa.
Ulimwengu lazima uzingatie hali mbaya ya hewa
Mohamed Adow, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Power Shift Africa, inayohusika na masuala ya hali ya hewa, anasema mwanzoni mwa mkutano wao, mfuko huo haukuwa hata kwenye ajenda, lakini sasa wameweka historia.
"Hii inaonesha kwamba mchakato huu wa Umoja wa Mataifa unaweza kufikia matokeo yake, na kwamba ulimwengu unaweza kutambua hali mbaya inazopitia nchi zilizoko hatarini, lazima izingatiwe kama soka la kisiasa," alisisitiza Adow.
Waziri wa Uchumi wa Kijani na Mazingira wa Zambia, Collins Nzovu ameliambia shirika la habari la Ufaransa, AFP kwamba amefurahishwa sana na makubaliano hayo. "Haya ni matokeo mazuri sana, kwa ajili ya Waafrika bilioni 1.3. Yanafurahisha kwa sababu kwetu sisi, mafanikio ya Misri yalikuwa yanategemea kile tutakachopata kutokana na hasara na uharibifu," alisema Nzovu.
Mfuko huo unahusisha athari nyingi zitokanazo na hali ya hewa, kuanzia madaraja na nyumba zilizosombwa na mafuriko, hadi kitisho cha kutoweka kwa tamaduni na visiwa vyote, hadi kuongezeka kwa kiwango cha bahari.
Mwaka huu majanga yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi kuanzia mafuriko makubwa nchini Pakistan hadi ukame mbaya unaotishia baa la njaa nchini Somalia, yalitiliwa mkazo zaidi katika nchi zilizokumbwa na maafa, ambazo tayari zilikuwa zikipambana na mfumuko wa bei pamoja na madeni yanayoongezeka.
Vipengele vingine bado vinajadiliwa
Baada ya kupiga kura, mazungumzo kuhusu vipengele vingine vya mazungumzo hayo yalisimamishwa, huku wajumbe wakipewa dakika 30 kusoma taarifa kuhusu hatua nyingine ambazo pia zinahitaji kupigiwa kura.
''Hivi ndivyo safari yetu ya miaka 30 hatimaye, tuna matumaini imepata mafanikio,'' alisema Waziri wa Mazingira wa Pakistan, Sherry Rehman, ambaye mara nyingi amekuwa akiongoza kundi la mataifa maskini zaidi duniani.
Rehman amesema theluthi moja ya taifa lake lilizama wakati wa msimu wa joto baada ya mafuriko makubwa, huku yeye na maafisa wengine wa Pakistan wakitumia kaulimbiu inayosema ''Kilichotokea Pakistan, hakitosalia Pakistan.''
Kwa upande wake Alex Scott, mtaalamu wa diplomasia katika taasisi ya mazingira ya E3G, anasema hiyo ni taswira ya kile kinachoweza kufanywa wakati mataifa maskini zaidi yakiungana kwa pamoja. ''Nadhani hili ji jambo kubwa sana kuwa na serikali zinazozungumza lugha moja, ili kufanyia kazi hatua ya kwanza ya jinsi ya kukabiliana na suala la uharibifu na hasara,'' alifafanua Scott.
Hata hivyo, Scott anabainisha kuwa kama ilivyo kwa fedha zote za hali ya hewa, ni jambo moja kuanzisha mfuko, na jambo jengine kuzipata fedha hizo zinazoingia na kutoka.
Ahadi za awali bado hazijatekelezwa
Ulimwengu wa nchi zilizoendelea bado haujatimiza ahadi yake ya mwaka 2009 ya kutoa dola bilioni 100 kila mwaka kwa ajili ya misaada mingine ya hali ya hewa, iliyoanzishwa kwa ajili ya kuzisaidia nchi maskini kukuza nishati ya kijani na kukabiliana na ongezeko la joto katika siku zijazo.
Harjeet Singh, mkuu wa mikakati ya kisiasa na kimataifa katika Mtandao wa Kimataifa wa Hali ya Hewa, anasema makubaliano hayo yanatoa matumaini kwa watu walioko hatarini zaidi kwamba watapata msaada wa maafa yatokanayo na hali ya hewa na kuyajenga upya maisha yao.
Ingawa Misri, ambayo ilikosolewa na pande zote ndiyo ilipendekeza kuanzishwa kwa mfuko mpya wa hasara na uharibifu, mpatanishi wa Norway amesema haikuwa kwa Wamisri peke yao, lakini nchi zote zilizofanya kazi pamoja.
Mjumbe wa hali ya hewa wa Ujerumani, Jennifer Morgan na Waziri wa Mazingira wa Chile, Maisa Rojas, ambao waliusimamia mpango huo hadi kwenye ajenda na hadi mwisho, walikumbatiana baada ya kupitishwa, na kisha wakapiga picha ya pamoja na kusema "ndiyo, tumefanikiwa!"
Soma zaidi: Guterres atoa wito wa kufikiwa makubaliano
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, mfuko huo awali ungetumia michango kutoka kwenye nchi zilizoendelea na vyanzo vingine binafsi na vya umma, kama vile taasisi za fedha za kimataifa.
Ingawa mataifa makubwa yanayoinukia kiuchumi kama vile China, hayangehitaji kuchangia hapo awali, chaguo hilo bado liko mezani na litajadiliwa katika miaka ijayo.
Hayo ni matakwa makubwa ya Umoja wa Ulaya na Marekani, ambazo zinasema kwamba China na wachafuzi wengine wakubwa kwa sasa wanaotajwa kuwepo katika nchi zinazoendelea, zina uwezo wa kifedha na zinawajibika kulipa.
(AP, DPA, AFP, Reuters)