041210 Cancun Klimafonds
6 Desemba 2010Kuanzia mwaka 2020 mfuko wa kimataifa kwa ajili ya mabadiliko ya tabia nchi utakuwa unagawa kiasi cha dola bilioni 100 kila mwaka , ili kupunguza kasi ya mabadiliko ya hali ya hewa pamoja na kudhibiti hali ya utoaji wa gesi zinazoharibu mazingira duniani. Katika mkutano wa umoja wa mataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi uliofanyika mjini Copenhagen mwaka 2009 kulikuwa na makubaliano ya kisiasa kuhusu kima hicho. Lakini hadi sasa haifahamiki , nani anapaswa kuchangia katika mfuko huo. Hili ni moja kati ya maswala kadha ambayo yanaleta mivutano katika mkutano huo wa mazingira mjini Cancun nchini Mexico, mkutano ambao unaendelea hadi hapo Desemba 10.
Uamuzi juu ya kuundwa kwa mfuko wa kimataifa imara wa kupambana na mabadiliko ya tabia nchi ifikapo mwaka 2020 tayari umefikiwa katika mkutano wa Kopenhagen. Dola bilioni 100 zitatolewa na mfuko huo kila mwaka kuazia mwaka 2020. Mjini Cancun , tunajaribu kwa mara ya kwanza kuweza kukubaliana , ni utaratibu gani tunaweza kuliangalia suala hilo, anasema hivyo mkuu wa sekretarieti ya umoja wa mataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi, Christina Figueres.
Mfuko huu ambao unajadiliwa hapa Cancun na ambao pia utakuwa sehemu ya mpango huo, unalengo la kutoa fedha kwa muda mrefu. Na maswali ambayo kwa sasa yanajadiliwa, ni iwapo mfuko huo uundwe hapa Cancun , na kisha ufanyiwe utaratibu wa kupangwa, kwa kuwa hakuna rais wa mfuko kama huu, na hilo linahitaji mipango ya kitaalamu na tahadhari. Ama kwanza iwapo kunahaja ya utaratibu wa kupanga na kisha hilo likikubalika na pande zote, ndio mfuko huo uundwe mwaka ujao.
Iwapo kutakuwa na mfuko wa dola bilioni 100 ambazo zitagawiwa kila mwaka , ni lazima kwanza serikali zitoe ridhaa yao. Kuna shauku halali kwa upande wa mataifa fadhili yenye viwanda, kama ilivyo pia kwa mataifa yanayofadhiliwa, mataifa yanayoendelea. Mataifa fadhili yanataka kupata uhakika, kwamba fedha hizo zitatolewa kwa ajili ya matumizi ya kupambana kweli na mabadiliko ya tabia nchi. Mataifa yanayofadhiliwa yanataka kuwa na uhuru wa kuamua kuhusu hatua zake za kitaifa na hakuna masharti yanyowekwa pamoja na ufadhili huo, kwa mfano katika masuala ya kisiasa. Katika majadiliano pia kuna suala la benki kuu ya dunia kuwa moja kati ya vyombo vinavyogawa misaada hiyo ya mfuko wa mabadiliko ya tabia nchi.
Pande zinazohusika katika mazungumzo haya zitaamua ni aina gani ya mfuko wa aina hiyo utaundwa. Tutapendekeza hilo kwa njia ya kitaalamu kabisa. Ni muhimu kwamba kila dola , kila euro inatumika vizuri. Kwa hiyo unahitaji kuendeshwa kwa njia kwamba unatoa matunda.
Anasema hivyo mwakilishi maalum wa benki kuu ya dunia katika mkutano huo wa mabadiliko ya hali ya hewa, Andrew Steer. Anaweka wazi kuhusu hilo, kwamba benki kuu ya dunia , ikiwa na uzoefu wa miaka 65 katika kutoa fedha kwa ajili ya maendeleo, inahisi inastahili kuchukua jukumu hilo, itakuwa ni heshima kubwa kwa taasisi hiyo, anasema.
Mwandishi : Helle Jeppesen / ZR / Sekione Kitojo
Mhariri: Aboubakary Liongo