1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waisraeli na Wapalestina waanza kurudia maisha ya kawaida

22 Mei 2021

Maelfu ya Wapalestina waliokimbia makwao, wameanza kurejea katika makaazi yao ambayo yameharibiwa pakubwa kufuatia mashambulizi kwenye Ukanda wa Gaza. Waisraeli vilevile wameanza kurudia maisha yao ya kawaida.

https://p.dw.com/p/3tnp5
Gaza | Palästinenser feiern Waffenruhe zwischen Israel und der Hamas
Picha: Mohammed Salem/Reuters

Kufuatia kudumishwa kwa makubaliano ya kusitisha vitabaada ya mashambulizi makali yaliyodumu kwa siku kumi na moja, hatimaye maelfu ya Wapalestina walioyatoroka makaazi yao wameanza kurudi kwenye makao yao.

Maelfu kwa maelfu ya wakaazi walionekana nje jana Ijumaa kwa mara ya kwanza baada ya siku nyingi wakitembelea majirani, wakiyaangalia majengo yaliyoporomoshwa, wengine wakielekea baharini na wengine wakiwazika wapendwa wao waliouawa wakati wa mashambulizi.

Lakini mjini Jerusalem, maafisa wa polisi wa Israel waliwatawanya waandamanaji waliowarushia mawe katika eneo tete lenye msikiti wa Al-Aqsa, wiki mbili tangu matukio kama hayo kuchochea makabiliano mabaya kuwahi kushuhudiwa kwa miaka mingi.

Polisi ya Israel imesema, maandamano pia yalitokea katika baadhi ya sehemu za Mashariki mwa Jerusalem na Ukingo wa Magharibi.

Biden: Suluhisho ni mataifa mawili

Maelfu ya Wapalestina washerehekea baada ya mapigano kusitishwa.
Maelfu ya Wapalestina washerehekea baada ya mapigano kusitishwa.Picha: Mohammed Talatene/dpa /picture alliance

Awali, rais wa Marekani Joe Biden aliwaambia Waisraeli kuacha kile alichokiita kuwa ‘mapigano ya kijamiii' mjini Jerusalem, huku akiahidi kuongoza juhudi za kuijenga upya Gaza.

Biden pia amesisitiza haja ya kuundwa mataifa mawili akisema ndiyo suluhisho pekee kwa mgogoro wa Mashariki ya Kati.

Waokoaji wamesema hawana vifaa vya kutosha wanaposaidia kutafuta manusura ambao huenda wamefunikwa kwenye vifusi.

Nazmi Dahdo mwenye umri wa miaka 70 amesema mashambulizi ya angani yaliyofanywa na Israel yaliharibu makaazi yake katika mji wa Gaza.

"Hatuna makao mengine. Nitaishi kwenye hema juu ya vifusi vya nyumba yangu hadi pale itakapojengwa upya,” amesema Dahdo ambaye ni mzazi wa watoto watano.

Israel na Hamas wadi ushindi

Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alisema mashambulizi ya Israel yaliwaua zaidi ya magaidi 200 ndani ya Gaza, wakiwemo makamanda wakuu 25 na kutaja hilo kuwa ufanisi wa kipekee.

Watawala wa Hamas pia walidai "ushindi”. "Tumewapa pigo kubwa ambalo litaacha makovu makubwa kwa Israel,” amesema mkuu wa kisiasa wa kundi hilo Ismail Haniyeh.

Hamas, Israel waanza makubaliano usitishaji mapigano

Haniyeh pia aliipongeza Iran kwa kuwasaidia na fedha na silaha.

Misri ndiyo ilisimamia makubaliano hayo yaliyojumuisha pia kundi kubwa la pili lenye silaha lenye misimamo mikali ya Kiislamu. Hiyo ni baada ya shinikizo za kimataifa.

Misaada ykwa wakaazi wa Ukanda wa Gaza

Hazina ya masuala ya dharura ya Umoja wa Mataifa ilisema tayari imetoa dola milioni 18 kuelekezwa kwenye juhudi za misaada ya kiutu ndani ya Ukanda wa Gaza. Umoja huo umesema msaada wa kifedha unahitajika Gaza.

Kwa jumla mashambulizi ya angani ya Israel tangu Mei 10, yalisababisha vifo 248, ikiwa ni pamoja na watoto 66. Na kuwajeruhi wengine 1,948. Wizara ya Afya imesema hayo. Wapiganani ni miongoni mwa waliouawa.

Kulingana na kundi la Hamas, majengo kadhaa yameporomoshwa na watu 120,000 wamepoteza makaazi.

Jeshi la Israel limesema wanamgambo wa Gaza walifyatua Zaidi ya makombora 4,300 kuelekea Israel lakini asilimia 90 ya makombora hayo yalizuiwa na mfumo wa ulinzi wa Israel.

Jamaa wa Kipalestina wakumbatiana wakishangilia kusitishwa mapigano Wapalestina
Jamaa wa Kipalestina wakumbatiana wakishangilia kusitishwa mapigano WapalestinaPicha: Mohammed Salem/Reuters

Makombora yaliyofyatuliwa na Hamas yalisababisha vifo vya  watu 12 ndani ya Israel, akiwemo mwanajeshi mmoja wa Israel. Watu wengine 357 walijeruhiwa.

Mnamo Alhamisi usiku, ofisi ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ilitangaza, usitishwaji mapigano bila masharti yoyote. Kundi la Hamas pia likathibitisha hayo.

Shirika la habari linalomilikiwa na serikali ya Misri limesema ujumbe wa maafisa wa usalama kutoka Cairo tayari wamewasili Gaza kuyafuatilia makubakiano hayo.

Viongozi mbalimbali ulimwenguni waliukaribisha mpango huo wa usitishaji vita.

(AFPE)