Israel, Wanamgambo wa Palestina wakubali kusitisha mapigano
21 Mei 2021Makubaliano ya kusitisha mashambulizi baina ya Israel na wanamgambo kutoka palestina yameanza kutekelezwa usiku wa kuamkia Ijumaa. Viongozi mbalimbali wamepongeza na kuyakaribisha makubaliano hayo ya kusitisha mashambulizi baina ya Israel na makundi mawili ya wanamgambo wa Palestina Hamas na jingine linaloshikilia itikadi kali za Kiislamu.
Rais wa Marekani Joe Biden ameyakaribisha makubaliano hayo na ameeleza kuwa yanatoa nafasi muafaka kupiga hatua mbele baada ya siku 11 ya mashambulizi hatari, na kwamba amejitolea kwa hilo.
Punde tu muda wa kuanza utekelezaji wa makubaliano hayo ulipofika (saa nane usiku, majira ya Mashariki ya Kati), wakaazi wengi wa gaza walimiminika mitaani wakipaza sauti zao wakisema Mungu ni Mkubwa. Ishara ya afueni baada ya mashambulizi makali yaliyowanyima nafasi ya kusherehekea Siku kuu ya Idd El-Fitr wiki iliyopita.
Wito watolewa suluhisho la kudumu litafutwe
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres pia ameyakaribisha makubaliano hayo. Amezitaka pande mbili husika Israel na viongozi wa Hamas kuheshimu makubaliano hayo huku akionmgeza kuwa jumuia ya kimataifa sharti itengeneze mpango unaowaunga mkono Wapalestina na kuimarisha taasisi zao.
Mwanadiplomasia mkuu wa Palestina Riad Al-Malki amesema usitishaji huo wa mashambulizi utawawezesha Wapalestina milioni 2 kulala usiku wa kuamkia Ijumaa. Lakini hautoshi kabisa. KWa hivyo ni lazima ulimwengu ulisuluhishe suala tete la mustakabali wa Jerusalem na taifa huru la Palestina liwepo.
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu Amani ya Mashariki ya kati Tor Wennesland amesema ameyakaribisha makubaliano hayo. Ametuma risala za rambirambi kwa wote walioathiriwa. Amezipongeza Misri na Qatar kwa juhudi zao kwa ushirikiano wa karibu na Umoja wa Mataifa kuaidia kurejesha utulivu. Amemaliza akisema kazi ya kuijenga Palestina sasa inaweza kuanza.
Waziri wa mambo ya nchi ze nje wa uingereza Dominic Raab pia ameyakaribisha makubaliano hayo kati ya Israel na Gaza. Kupitia ukurasa wake wa Twitter amesema ni lazima pande zote kudumisha makubaliano hayo na zimalize machafuko ya mara kwa mara na vifo vya raia. Ameongeza kuwa uingereza inaunga mkono juhudi zinazoleta Amani.
Makubaliano yalisimamiwa na Misri
Rais wa Misri Abdel Fattah Al-Sissi kupitia ukurasa wake wa Twitter amempongeza Rais Joe Biden kwa mchango wake kuwezesha juhudi za Misri za kuhimiza usitishaji vita Gaza kufaulu.
Al-Sissi amesema yeye na Rais Biden waliona haja ya dharura iliyohitajika kati ya pande zote pamoja na diplomasia kudhibiti mzozo huo.
Israel na wanamgambo wa Palestina walitangaza usitishaji mashambulizi Ijumaa usiku wakilenga kumaliza mgogoro mbaya zaidi kuwahi kutokea kati yao ndani ya miaka saba iliyopita.
Makubaliano hayo yalisimamiwa na Misri na yamejiri baada ya miito ya kimataifa kutaka machafuko hayo ambayo yamedumu kwa siku 11 kusitishwa.
Taarifa kutoka kwenye ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ilisema baraza la usalama la nchi hiyo limekubali kwa pamoja pendekezo la maafisa wote wa kiusalama, kuridhia wito wa Misri wa kuwepo usitishaji vita bila ya masharti.
Kundi la Hamas na wanamgambo wa itikadi za dini ya Kiislamu pia walithibitisha usitishaji wa mashambulizi.
Tangu mzozo huo ulipoanza, maafa makubwa yameshuhudiwa ikiwa ni pamoja na zaidi ya Wapalestina 200 kuuawa kufuatia mashambulizi ya angani ya majeshi ya Israel katika Ukanda wa Gaza.
Zaidi ya watu 10 pia wameuawa ndani ya Israel kufuatia maelfu ya makombora yaliyofyatuliwa na makundi mawili makubwa ya wanamgambo yaliyoko Gaza- Hamas na kundi la Kiislamu la Jihad.