Waislamu zaidi ya 100 wakamatwa Pakistan
17 Agosti 2023Wakristo wanaoishi katika mji wa Jaranwala kwenye wilaya ya Faisalabad, kwa haraka walikimbilia mahali salama wakati kundi hilo la waislamu lilipoanza kuwavamia. Polisi imesema hakuna mtu yeyote aliyeuwawa wala kuumia katika kisa hicho.
Uharibifu uliosababishwa na uvamizi huo ulionekana baada ya baadhi yao kuamua kurejea nyumbani. Kanisa moja lilichomwa moto na mengine manne kuharibiwa na nyumba kadhaa zilichomwa moto na nyingine pia kuharibiwa vibaya.
Watu 13 wameuwawa katika mapigano Pakistan
Shazia Amjad amesema alikuwa amekaa nyumbani kwake aliposikia kwamba kundi la watu linakuja kuchoma nyumba zao pamoja na makanisa. Amesema vitu vyao vya ndani ya nyumba kama makochi yalichomwa, huku vingine vikiibwa na watu hao. Kwa sasa yeye na wenzake hawajui pa kwenda au kile cha kufanya baada ya kupoteza makaazi yao.
Padri wa eneo hilo Khalid Mukhtar aliliambia shirika la habari la AFP kwamba makanisa 17 yalishambuliwa na nyumba yake binafsi kuharibiwa.
Waislamu wanadai wakristo walikikashifu kitabu kitukufu cha Quran
Ghasia zilianza pale kundi dogo la waislamu lilipodai kumuona kijana mmoja wa Kikristo Raja Amir, na rafiki zake wakichana kurasa za kitabu kitakatifu cha Quran na kuandika maneno ya kuikashifu dini katika kurasa nyengine za kitabu hicho. Polisi hadi sasa imesema inajaribu kumsaka na kumkamata Amir ambaye hajulikani aliko kujua iwapo kweli alikichana kitabu hicho au la.
Katika hatua ya kutuliza hali, viongozi kadhaa wa kidini wamewasili mjini Jaranwala kusaidia kuleta uwiano na maridhiano kati ya dini hizo mbili, huku polisi na wanajeshi wakiendelea kushika doria katika eneo hilo.
Mamlaka pia imeamuru kufungwa kwa shule zote mjini humo, kupiga marufuku mikutano ya hadhara na kufunga ofisi kwa wiki nzima ili kuzuwia vurugu zaidi.
Hali inayoendelea huko kwa sasa imekosolewa na wengi kitaifa huku kaimu Waziri Mkuu Anwaarul-ul-Haq Kakar akiamuru polisi kuhakikisha kuwa wale wanaoleta vurugu wamekamatwa. Mkuu wa polisi wa mji wa Jaranwala Rizwan Khan amethibitisha idadi ya waliokamatwa kuwa 129 na kusema kwamba kwa sasa hali imeshadhibitiwa.
Makundi ya kutetea haki za binaadamu yakosoa yanyoendelea Pakistan
Makundi ya kutetea haki za binaadamu ya ndani na nje ya pakistan pia yamepaza sauti zao juu ya tukio hili.
Shirika la Kimataifa la haki za binaadamu, Amnesty International limetoa wito wa kufutwa kwa sheria ya kutenda kufuru nchini Pakistan, huku Marekani ikitaka uchunguzi huru na wa haraka kufanywa dhidi ya tukio hilo na kuwatolea wito wananchi kuwa watulivu.
Pakistan: Umati wenye hasira wamuua mtu anayeshutumiwa kuinajisi Quran
Chini ya sheria ya kufuru Pakistan, mtu yeyote atakaepatikana na hatia ya kutenda matendo ya kukashifu uislamu au viongozi wa dini ya kiislamu anaweza kuhukumiwa kifo.
Bado hukumu ya kifo haijawahi kutolewa pakistan dhidi ya makosa haya lakini madai tu ya tukio hilo husababisha maandamano na kufanya makundi ya watu kuanza kutenda visa vya vurugu kwa kuwapiga watu na kuwaua.
Chanzo: ap/afp