1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafanyabiashara watakiwa kuunga mkono vita dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa

Aboubakary Jumaa Liongo25 Mei 2009

Jijini Copenhane Demark kunafanyika mkutano wa kimataifa wa wadau wa sekta ya biashara kujaribu kukusanya nguvu kungana mkono sera za kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa.

https://p.dw.com/p/HxAO
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moonPicha: AP


Mkutano huo uliyoanza jana ambao utamalizika kesho unawajumuisha wakuu katika sekta ya biashara zaidi ya 500 kutoka kote duniani.


Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban-Kin-moon ametoa wito kwa sekta ya viwanda kutoa mchango mkubwa katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa, kwa kukubaliana na mipango ya serikali ya kuvitaka kupunguza utoaji wa gesi ya carbon, na siyo kufanya mikakati ya kupinga.


Wakuu wa sekta ya biashara wanajadiliana ni vipi wataweza kuongeza uzito wao katika kuhakikisha unafikiwa mkataba mpya wa kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa kuchukua nafasi ya ule wa Kyoto.Mkataba huo mpya unatarajiwa kufikiwa katika mkutano wa Umoja wa Mataifa wa hali ya hewa utakaofanyika Decemba mwaka huu huko huko Copenhagen Denmark.


Amewaambia wale wote wenye dhana na fikra za kupinga kufikiwa kwa mkataba huo kuwa, fikra hizo zimepitwa na wakati, na kwamba biashara nzuri ni ile inayozalisha fedha huku ikilinda mazingira.


Naye Waziri wa Nishati na Mazingira wa Denmark Connie Hedegaard, ambaye atakuwa mwenyeji wa mkutano ujayo wa Umoja wa Mataifa, amesema biashara inayofanywa na nchi yake ya usafirishaji nje wa mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia upepo umethibitisha kuwa mapambano dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa ni kitu ambacho kinaweza kuwa na faida kubwa kibiashara.


Kwa upande wake Makamu wa zamani wa rais wa Marekani Al Gore amewaambia wafanyabiashara hao kuwa wakati ndiyo huu wa kufikiwa kwa mkataba mpya na kwamba hakauna tena muda wa kupoteza.


Amesema kuwa sekta ya wafanyabishara na viongozi wa mataifa ni lazima washirikiane katika kuilinda dunia na mabadiliko makubwa ya hali ya hewa, na kuongeza kuwa dunia kwa sasa inakabiliwa na majanga matatu yanayoshabihiana.


Al Gore in Kopenhagen
Makamu wa rais wa zamani wa Marekani Al GorePicha: AP

´´Kwa wakati huu hapa duniani tunakabiliwa mizozo mitatu inayofanana.mzozo wa hali ya hewa, mzozo wa kiuchumi na mzozo wa nishati.Kuna kitisho kinachofanana katika mizozo yote hiyo mitatu, ni mahitaji yetu kupita kiasi cha nishati inayotoa gesi aina ya carbon´´


Wakati Umoja wa Mataifa ukiwa na matumaini ya kufikiwa kwa mkataba madhubuti, kutokana na ule wa Kyoto, tayari Umoja wa Ulaya kwa upande wake umesema kuwa utapunguza utoaji wa gesi hiyo ya carbon inayoharibu mazingira kwa asilimia 20 ifikapo mwaka 2020 na kwamba itaongeza hadi kufikia asilimia 30, iwapo lakini, nchi nyingine nazo zitaahidi kufikia lengo hilo.


Rais wa zamani wa Marekani George Bush alikataa kutia saini kuridhia mkataba wa Kyoto, akihofu kuwa utaukwaza uchumi wa nchi hiyo.


Lakini mridhi wake, Rais Barack Obama ameahidi kuwa Marekani itakuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ongezeko la ujoto duniani.


Waandaji wa mkutano huo wanasema kuwa ajira mpya milioni kadhaa zitapatikana Marekani pekee, kwa kuamua kutegemea nishati mbadala na endelevu au kupunguza utoaji wa gesi ya carbon, kama vyanzo wa umeme.


Rais wa kamisheni ya Umoja wa Ulaya Jose Manuel Bbarroso amesema kuwa uwekezaji kama huo unaweza pia kutoa ajira milioni kadhaa barani Ulaya, kwani mabadiliko katika sekta yoyote hufungua pia njia kwa nafasi kubwa za kiuchumi.


Nje ya mkutano huo wa Denmark zaidi ya waandamanaji 300 wanaopinga sera za kibepari wamekuwa wakishiriki kwa namna yao.


Msemaji wa Polisi katika jiji la Copenhagen Flemming Steen Munch amesema kuwa kiasi cha vijana 40 wamekatwa kutokana na vurugu


Mwandishi:Aboubakary Liongo

Mhariri:Mohamed Abdul-rahman